BASI LAUA WATU WANNE NA KUJERUHI 35


Ajali nyingine imetokea nchini na safari hii imehusisha basi la Air Bus lililokuwa likitoka  Dar es Salaam kwenda  Tabora.
Ajali hiyo iliyotokea mkoani Morogoro jana, ilisababisha  vifo vya watu wanne na majeruhi wapatao 35.
Imetokea siku chache tangu ajali ya hivi karibuni iliyoua watu 39, iliyohusisha magari matatu wilayani Butiama, Mkoa wa Mara.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Leonard Paul alisema ajali hiyo ilitokea jana saa 5: 45 asubuhi   katika eneo la Daraja la Mkange kati ya Kijiji cha Berega na Kiegeya wilayani Kilosa.
Waliopoteza maisha ni wanawake watatu na mwanamume,  ambao walikufa papo hapo na majina yao hayakupatikana. Majeruhi walikimbizwa   Hospitali ya Misheni ya Berega.
Kamanda  alisema basi  hilo lenye namba za usajili T106  AGB,  lilikuwa likitoka  Dar es Salaam kwenda mkoani  Tabora.
Alisema kutokana na mwendo kasi, liliacha  njia na kwenda kutumbukia korongoni  kwenye  daraja la Mkange lililopo kwenye  barabara kuu ya Morogoro- Dodoma.
Dereva wa basi hilo, Bilal Seif alitoweka  eneo hilo na Polisi inamsaka achukuliwe hatua za kisheria.
Mganga wa zamu wa Hospitali ya Misheni ya Berega wilaya ya Kilosa, Alfred Chiponda, alisema kati ya majeruhi,  10 ni wanawake, sita ni watoto na 19 ni  wanaume ambao wameumia vibaya kwa kuvunjika sehemu mbalimbali mwilini.
Walioumia vibaya wamehamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro.
Mashuhuda wa ajali hiyo, walisema dereva wa basi hilo  alikuwa kwenye mwendo kasi na alitaka kupita gari lingine, lililokuwa mbele yake na kupoteza mwelekeo, hali iliyosababisha gari hilo kuacha njia na kupinduka eneo  la darajani.

No comments: