Siku chache baada ya majambazi kuvamia
Kituo Kikuu cha Polisi wilayani Bukombe mkoani Geita, kuua askari wawili na
kuiba silaha za moto, watu wasiofahamika wamewajeruhi askari watatu waliokuwa
doria kwa kuwarushia kitu kinachosadikiwa kuwa ni bomu.
Askari hao kwa sasa wamelazwa katika
Hospitali ya Mkoa wa Ruvuma iliyopo mjini Songea wakitibiwa majeraha.
Tukio hilo limeripotiwa kutokea usiku wa
kuamkia jana majira ya saa moja na nusu jioni katika kata ya Msufini karibu na
daraja la Matarawe, wilayani Songea.
Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai
(DCI), Issaya Mngulu amethibitisha kwa njia ya simu kutokea kwa tukio hilo,
ingawa alishindwa kuingia kwa undani akisema alikuwa njiani kwenda eneo la
tukio akitokea mkoani Mbeya.
Hata hivyo, mwandishi ameweza kubaini
waliojeruhiwa kuwa ni WP. 10399 PC Felista aliyejeruhiwa mguu wa kulia kwenye unyayo na pajani, G 7351 PC Ramadhani
aliyejeruhiwa mguu wa kulia karibu na goti na tumboni upande wa kulia na G.
5515 PC John aliyepata majeraha katika mguu wa kulia chini ya goti na jeraha
dogo tumboni.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Ruvuma,
Dk Daniel Malekela, akizungumzia tukio hilo alikiri kupokea majeruhi na kueleza
kuwa ametoa vipande vya bati na misumari katika majeraha ya askari hao na mpaka
sasa wanaendelea na matibabu.
Habari zaidi zinasema jeshi la polisi
mkoani humo kwa kushirikiana na maofisa wengine kutoka makao makuu ya jeshi,
wanaendelea na uchunguzi, ikiwa ni pamoja na kujua chanzo cha tukio hilo. Bomu
hilo la kutupwa kwa mkono inasadikiwa limetengenezwa kienyeji.
Kutokana na tukio hilo, Mkuu wa Mkoa wa
Ruvuma, Saidi Mwambungu ameelezea kusikitishwa na kitendo hicho cha wahalifu
kujeruhi askari kwa makusudi na amesema Serikali kupitia vyombo vyake vya
ulinzi na usalama itahakikisha wanawasaka na kuwakamata.
No comments:
Post a Comment