ALIYEMBAKA MFANYAKAZI WA NDANI JELA MIAKA 30



Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani imemhukumu kwenda jela miaka 30 mlinzi wa Shule ya Sekondari ya Mbwawa Steven Solomon (29) kwa kosa la kumbaka mfanyakazi wake wa nyumbani mwenye umri wa miaka 16.
Akitoa hukumu hiyo Hakimu wa mahakama hiyo, Harieth Mwailolo alisema iliridhika na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na upande wa chini ya mwendesha mashitaka Salim Msemo.
Ilielezwa kuwa mtuhumiwa alitenda kosa hilo Januari 30 mwaka huu huko Mbwawa Mtongani Kata ya Kilangalanga Tarafa ya Mlandizi wilayani Kibaha.
Mlinzi huyo alifanya unyama huo wakati mkewe akiwa amelazwa Kituo cha Afya cha Kilangalanga.
Mahakama ilielezwa kuwa mtuhumiwa baada ya kufanya tukio hilo alikutwa na mjumbe wa shina namba 13 Kilangalanga, Mwajuma Rajabu na mashahidi wengine na mlalamikaji na kukubaliana kuwa atamlipa kiasi cha Sh  milioni moja kwa ahadi ya kila mwezi angetoa kiasi cha Sh 70,000 makubaliano ambayo yalifanywa Aprili Mosi mwaka huu.
Mlinzi huyo alijutia kosa alilofanya na kuiomba Mahakama kumpunguzia adhabu hata hivyo Mahakama iliamuru  atumikie kifungo cha miaka 30 jela.

No comments: