ABAKWA, ANYONGWA KISHA MWILI WAKE KUTUPWAMkazi wa Kijiji cha Bupu wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani, Forodesi Ntabegera (30) ameuawa kwa kubakwa, kisha kunyongwa na watu wasiojulikana, kisha mwili wake kutupwa kichakani.
Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Pwani, Athuman Mwambalaswa alieleza kuwa Ntabegera alinyongwa na watu hao kwa kutumia kitenge chake alichovaa.
Mwambalaswa alisema Septemba 9 mwaka huu saa 8:00 mchana wakazi wa kijiji hicho, walifanya msako wa kumtafuta Ntabegera baada ya kupotea Septemba 8 mwaka huu.
“Baada ya msako huo kufanyika, mwili wa marehemu ulikutwa kwenye kichaka umbali wa mita 30 kutoka barabarani, ambapo mwili wake ulimwagiwa unga kichwani na mgongoni,” alisema Kamanda.
Kamanda alisema wauaji walitumia mfuko aliobebea unga Ntabegera akitokea kusaga, kumvisha miguuni kisha mwili wake waliulaza kifudifudi. Polisi inawasaka wahusika.

No comments: