WATEKELEZA AGIZO LA KIKWETE KUJENGA MAABARA


Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, mkoani Singida imeanza utekelezaji wa programu ya ujenzi wa maabara katika shule za sekondari ikiwa ni agizo lililotolewa na Rais Jakaya Kikwete kwa halmashauri zote nchini.
Kaimu Mkurugenzi wa Wilaya ya Iramba, Focus Marwa alisema hayo ofisini kwake wakati akizungumza na gazeti hili na kuongeza kuwa hadi sasa shule za sekondari 19 zinakaribia kukamilisha ujenzi huo.
Alisema hatua waliyofikia ni nzuri kwani wanaelekea ukingoni ingawaje  wanakabiliwa na tatizo la  rasilimali ambazo zingewezesha kukamilisha kabisa mpango huo.
“Mpango huu ni kwa shule zote za sekondari katika wilaya hii…hatuna rasilimali za kutosha lakini tunaendelea kuhamasisha jamii ichangie ingawaje mchango wa halmashauri kutokana na mapato yake ya ndani ni muhimu pia,” alisema Marwa.
Alisema mkakati wa ujenzi wa maabara pia ni mkakati wa mkoa kwamba kila halmashauri itekeleze ujenzi wa maabara ili kuwasaidia wanafunzi kuweza kufanya vizuri katika mafunzo ya vitendo.
Marwa alisema programu hiyo inatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi huu, lakini pia wanaendelea kuihamasisha jamii kuamka na kuchangia ili kumalizia ujenzi huo.
Akizungumzia tatizo la kukosekana kwa barabara katika Kijiji cha Tutu aliwataka wananchi wa eneo hilo kufahamu kuwa ujenzi wa barabara hiyo hauko katika bajeti ya maendeleo ya halmashauri ya mwaka huu.

No comments: