WAOMBA ELIMU YA UFUGAJI NYUKI KISASA


Wakulima wilayani hapa, ambao pia ni  wafugaji wa nyuki wamewataka wataalamu wa mifugo kuwatembelea vijijini kutoa  elimu juu ya ufugaji nyuki kwa njia ya kisasa.
Wakulima hao walitoa kauli hiyo kwa nyakati tofauti  kwenye  Maonesho ya Wakulima ngazi ya vijiji yaliyofanyika  juzi,  Kata ya Diongioya, Tarafa ya Turiani wilayani humo.
Wakulima  kutoka vijiji 26  vya Tarafa ya Turiani na Mvomero  walipata fursa ya kushiriki  maonesho hayo maalumu yaliyoandaliwa na Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (Mviwata).
Hivyo walisema, ufugaji wa nyuki hauna gharama kubwa na wanachokikosa ni kupata elimu ya ufugaji wa kisasa utakaowaletea kipato chenye tija.
Wakulima hao walisema, wanachokihitaji ni kupatiwa elimu ya ufugaji nyuki kwa njia ya kisasa ambayo itawasaidia  katika suala la  kutunza mazingira ya misitu ya asili.
Mkulima na mfugaji wa nyuki wa Kijiji cha Hembeti, Bakari Shaaban, alisema kuwa licha ya kuendesha kilimo cha mpunga katika bonde la Mkindo, pia ameamua kufuga nyuki na kwamba mazao ya asali yamekuwa yakiwapatia kipato wakati huu ambao soko la mpunga limedorora.
Hata hivyo alisema, kufuatia wakulima wengi katika kijiji na kata hiyo ya Hembeti kujitokeza kufuga nyuki, mahitaji yao makubwa ni kupatiwa utaalamu wa ufugaji wa kisasa na kupata aina bora ya mizinga ya kufugia nyuki.
Kwa upande wao, wakulima wa Kijiji cha Dihinda, katika Kata ya Hembeti, Amina Ally pamoja na Omary Athuman kwa nyakati tofauti walisema, ukosefu wa soko la mazao kumetoa mwanya kwa walanguzi kuwalalia kwa kununua mazao yao kwa bei ndogo.

No comments: