WANAFUNZI WATUMIA VISODA NA MABUA DARASANI

Upungufu wa vitabu, vifaa vya kufundishia na kuhesabia kwa watoto wa darasa la awali kwa baadhi ya shule za msingi katika Halmashauri ya Iramba, mkoani Singida unasababisha wanafunzi kutumia mabua, visoda na vijiti kwa ajili ya kuhesabia.
Aidha, walimu wakuu wa shule mbalimbali za msingi wilayani hapa wanaiomba serikali kutoa ruzuku kwa watoto wa darasa la awali kwa kuwa huduma zao haziwezi kutenganishwa na  madarasa mengine.
Akizungumza na gazeti hili, Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Kizega, Elisante Gyuzi alisema sehemu kubwa, shule yake imekuwa ikipata vifaa mbalimbali kutoka kwa wahisani. 
Alisema kulingana na sera ya elimu ni lazima madarasa ya awali yawe maalumu, yawe na vyoo na madarasa ya kujitegemea kwa ajili ya watoto hao wadogo.  
“Kwa mfano, hapa shuleni kwangu lipo darasa ambalo lilikarabatiwa na wahisani na pia kutupatia vifaa mbalimbali ambapo imepunguza ile hali ya watoto kubeba vijiti ama mabua kwa ajili ya kuhesabia,” alisema. 
Shule ya msingi Kizega ni maalumu kutokana na kuwa na wanafunzi wenye mahitaji muhimu.
“Nawashukuru wakazi wa eneo hili ambao kwa nguvu moja wameelimishwa na kufahamu umuhimu wa elimu ambapo katika kuonesha jitihada zao wanafyatua tofali ili kujenga darasa la watoto wa awali,” alisema.
Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Tutu, Rebecca Pyuza alisema elimu ya awali shuleni hapo ni changamoto kubwa kwani hata mwalimu anayefundisha watoto hao ni wa kujitolea ambaye awali alikuwa mwalimu lakini baadaye alipumzishwa kabla ya shule kuamua kumtumia. 
Kwa upande wa Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Kisiriri, Gerson Mkoma alisema shuleni hapo watoto wa awali hutumia visoda, mabua na vijiti kwa ajili ya kuhesabia huku michoro  mingine wakisaidiwa na walimu wao.
Alisema shule hiyo haijawahi kuwa na vifaa maalumu kwa ajili ya mafunzo shuleni hapo na kuiomba serikali kuzikumbuka hasa shule ambazo ziko pembezoni ama vijijini zaidi.

No comments: