WAMAREKANI WAONESHA NIA KUWEKEZA EPZAWawekezaji wa Marekani wameonesha nia ya kutaka kuwekeza kwenye maeneo  ya Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji nchini (EPZA).
Mkurugenzi Mkuu wa EPZA, Dk Adelhelm Meru alisema hatua hiyo, inadhihirisha matunda ya kongamano la masuala ya biashara, lililofanyika Marekani  mwezi huu yanaanza kuonekana. 
Kongamano hilo lilifanyika baada ya Rais Jakaya Kikwete kushiriki mkutano wa Marais wa Afrika na Rais Barack Obama wa Marekani jijini Washington D.C.
Kongamano hilo lililojulikana kama ‘Doing Business in Tanzania’ liliandaliwa na EPZA, Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC) na Kituo cha Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) kwa kushirikiana na Corporate Council on Africa ya Marekani.
“Katika siku chache baada ya kurejea, tumepata kampuni tatu ambazo zimeleta maombi ya nia ya moja kwa moja kuwekeza katika maeneo maalumu,” alisema.
Alisema mamlaka imepokea maombi yanayotaka kuwekeza katika maeneo ya kuongezwa thamani zao la ngozi, teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama) na ujenzi wa miundombinu katika maeeneo maalumu ya mamlaka.
Akifafanua, alisema matarajio yaliyopo kwa sasa ni kuendelea kupata wawekezaji wengi kutoka nchi hiyo, kwa vile kongamano hilo liliipa nafasi nzuri Tanzania kutangaza fursa zilizopo nchini.
Rais Jakaya Kikwete aliongoza ujumbe wa Tanzania katika kongamano hilo kubwa. “Walionesha nia ya kutaka kuwekeza katika maeneo ya viwanda vya kuongeza thamani mazao ya Kilimo na uzalishaji nishati,” alifafanua Dk Meru.
Alitaja maeneo mengine kama utafiti wa gesi na mafuta, utoaji wa huduma kwa kampuni za utafutaji mafuta na gesi katika Bahari ya Hindi.
Kongamano hilo lilihudhuriwa na watu zaidi ya 400 na wafanyabiashara wa Tanzania walikutana na wenzao wa Marekani na kuzungumza biashara.

No comments: