AJIFUNGUA WATOTO WANNE, HOSPITALI 2 NA SIKU MBILI TOFAUTI

Mkazi wa Kijiji cha Lupili wilayani Misungwi Mkoa wa Mwanza, Tecla Kazimili (24), amejifungua watoto wanne, watatu wa kike na mmoja wa kiume kwa njia ya kawaida katika hospitali mbili tofauti na siku mbili tofauti. 
Katika hospitali ya kwanza, ambayo ni zahanati ya Kijiji cha Lupili Agosti mosi mwaka huu, Tecla alionekana ana ujauzito wa mtoto zaidi ya mmoja ambapo wakati wa kujifungua, alizaliwa wa kiume akiwa na kilo 1.6, lakini kwa bahati mbaya alikufa. 
Hata hivyo, wakunga walishuhudia mzazi huyo akiendelea kuwa na dalili ya kujifungua mtoto mwingine, lakini akawa amegoma kupita katika njia.  
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Marko Mwita, alisema baada ya kutokea kwa hali hiyo, alipigiwa simu kuombwa msaada.  
“Baada ya kupokea taarifa hiyo majira ya usiku, nilituma gari la wagonjwa kukimbilia kwenye zahanati hiyo iliyopo umbali wa kilometa 60 na kumleta mama huyo katika Hospitali ya Wilaya kwa huduma zaidi,” alisema.  
Alisema alipofikishwa hospitalini hapo, Tecla aliendelea kujifungua mpaka kesho yake hatimaye idadi ya watoto ikafikia wanne. 
“Hili ni tukio la kwanza katika hospitali hii ya Wilaya, mtu kujifungua watoto wanne, ni matukio yanayotokea mara chache, lakini tunamshukuru Mungu mzazi anaendelea vizuri huku watoto wake watatu, wote wa kike kila mmoja akiwa na uzito wa kilo mbili,” alisema.  
Dk Mwita alisema watoto hao wanahitaji uangalizi na msaada wa hali ya juu, kwani ni rahisi kupata maambukizi. 
Alitoa mwito kwa jamii kumsaidia mama huyo, kwani watoto hao wanahitaji msaada wa hali na mali kwa kuwa maziwa ya mama pekee hayatawatosheleza.  
Akizungumzia historia yake ya uzazi, Tecla alisema watoto hao ni uzazi wake wa nne na katika ule uliopita, watoto wote aliowazaa walifariki dunia katika umri tofauti, lakini wa utoto. 
“Kitendo cha watoto kufa baada ya kufikisha umri fulani, kilimfanya mume wangu anifukuze, nikalazimika kurejea nyumbani kwetu ambapo nilipewa ujauzito na kijana mwingine,” alisema. 
Alisema wakati anahudhuria kliniki, alielezwa kwamba alikuwa na zaidi ya mtoto mmoja baada ya kutoa taarifa kuwa anaona  tabia ya ujauzito huo ni tofauti na uzazi wake uliopita.   “Namshukuru Mungu kwa kunipatia watoto hawa na naiomba Serikali inisaidie kuwatunza ili wakue vizuri kwani peke yangu siwezi,” alisema. 
Kwa mujibu wa Tecla, aliumwa uchungu kwa siku tatu na alimaliza kujifungua Agosti 2. 

No comments: