WAIOMBA MAHAKAMA KUTUPILIA MBALI OMBI LA PONDA

Upande wa Jamhuri katika ombi la Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, Shekhe Issa Ponda umeiomba Mahakama kutupilia mbali ombi hilo kwa kuwa halijawasilishwa kisheria.
Katika ombi lake, Shekhe Ponda anaiomba Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam iitishe mwenendo wa kesi ya uchochezi inayomkabili katika Mahakama ya Morogoro, ikague mwenendo huo na kutoa maelekezo, ikiwemo kusimamisha kesi hiyo isiendelee kusikilizwa.
Akiwasilisha hoja jana, Wakili Mwandamizi wa Serikali Bernard Kongola alidai kuwa  mahakama haiwezi kukubali kusikiliza ombi hilo pia halijawasilishwa kisheria kwa kuwa hati ya kiapo inayoliunga mkono ina mapungufu ya kisheria ambayo hayawezi kurekebishika.
Alibainisha mapungufu hayo kuwa ni baadhi ya taarifa zilizopo kwenye hati ya kiapo hazijaelezwa zimetoka wapi kama inavyotakiwa kisheria pia hati hiyo ina maombi ambapo kisheria inatakiwa kuwa na hoja na hairuhusiwi kuwa na maombi.
Aliendelea kudai kuwa, hawajataja kifungu cha sheria kinachoiwezesha Mahakama kuwa na uwezo wa kusikiliza ombi kama hilo pia vifungu walivyotumia katika ombi lao haviiwezeshi Mahakama kusimamisha mwenendo wa kesi ya Mahakama ya Morogoro.
Aidha alidai ombi kama hilo lilitolewa mbele ya Majaji wengine wa Mahakama hiyo na kutolewa uamuzi hivyo Mahakama haiwezi kusikiliza ombi hilo.
Jaji Lawrence Kaduri aliahirisha kesi hiyo hadi Septemba Mosi mwaka huu ambapo Wakili Nassoro Juma anayemuwakilisha Shekhe Ponda atajibu hoja hizo za pingamizi la awali.
Ponda anakabiliwa na kesi ya uchochezi na kukiuka amri ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, iliyomtaka kutotenda kosa kwa mwaka mmoja, na kutotoka nje ya Mkoa wa Dar es Salaam bila kibali cha Mahakama. 
Awali Shekhe Ponda aliwasilisha ombi kwa Mahakama Kuu  kufanya marejeo ya uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro, uliokataa kumfutia mashitaka ya kukiuka amri ya Mahakama hata hivyo ombi hilo lilikatiliwa.

No comments: