WABUNGE WAKATAA KATIBA MPYA ISIWABANE



Baadhi ya wabunge wa Bunge Maalum la Katiba, wamependekeza kuondoa kwenye rasimu ya Katiba mpya, kipengele kinachotaka wananchi wapewe uwezo kisheria, kuwaondoa wabunge wao wasioweza kutatua kero za wapigakura wao, badala ya kusubiri mpaka baada ya Uchaguzi Mkuu. 
Sambamba na hilo, wabunge hao pia wameondoa utaratibu wa viti maalumu wa sasa, na kupendekeza utaratibu mwingine ambao wananchi watakuwa na uwezo wa kuwachagua wabunge
wanawake wa viti maalumu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mwenyekiti wa Kamati Namba Tano, Hamad Rashid Mohamed, alisema mapendekezo hayo ni sehemu tu ya mabadiliko yanayopendekezwa na wajumbe wengi wa kamati yake, walipojadili Sura ya Tisa ya Rasimu ya Mabadiliko ya Katiba.
Alisema asilimia 70 ya rasimu hiyo wameikubali, lakini wamependekeza maboresho mengi, ambayo hayabadilishi maudhui ya rasimu hiyo. 
Sura hiyo ya Tisa ya rasimu iliyoandaliwa na Tume iliyokuwa chini ya Jaji Joseph Warioba, inazungumzia   kuundwa kwa Bunge la Jamhuri ya Muungano na madaraka yake, na sehemu ya pili ya sura hiyo, inaelezea kuhusu uchaguzi wa wabunge.
Katika sehemu hiyo ya uchaguzi wa wabunge, ndani yake wapigakura wamepewa haki ya kumwajibisha mbunge, iwapo ataunga mkono sera zinazoenda kinyume na maslahi ya wapiga kura au ya Taifa. 
Pia, Mbunge huyo katika rasimu inayojadiliwa, imependekezwa aondolewe iwapo atashindwa kuwasilisha au kutetea kwa dhati, hoja zinazotokana na kero za wapigakura wake, kuacha kuishi au kuhamisha makazi yake kutoka eneo la jimbo la uchaguzi kwa zaidi ya miezi sita bila sababu ya msingi.
Akielezea hoja zilizotolewa na wabunge wa kamati yake katika kubadilisha sehemu hiyo ya rasimu, Mwenyekiti huyo alisema, “hii ikiachwa italeta vurugu katika nchi kwa sababu hakuna kigezo cha kumpima mbunge, hili linachanganya na utekelezaji wake ni mgumu na itakuwa chanzo cha vurugu katika Katiba na kwenye Katiba haitakiwi kuwe na ugumu wa jambo…sasa tumeona tukiondoe.”
Mohamed alisema kwenye Kamati yake, kumetokea mikiki mingi wakati wa kujadili rasimu hiyo, ambapo wajumbe wengi wametaka utaratibu wa kuwapata wabunge wanawake wa
viti maalumu ubadilishwe, na uwe ambao wananchi ndiyo watawapima. 
“Viti maalumu wapo waliotaka viondolewe, lakini wengine wakasema kwa sababu ya kutaka kuongeza usawa wa jinsia wa asilimia 50 kwa 50, viti maalumu viachwe lakini tukakubalianatutafute dirisha (utaratibu) jingine ambapo wananchi ndiyo watawapima wabunge hao, na sio utaratibu wa sasa ambao unakuta familia moja imetoa wabunge wanawake zaidiya wawili,” alisema.
Hata hivyo, alisema utaratibu huo walioupendekeza, watautaja bungeni na wabunge ndiyo wataamua uwe vipi. Alikataa kuutaja kwa sasa, akisema atamaliza utamu wake.
Kuhusu ukomo wa vipindi vya ubunge, wamekubaliana chama cha siasa ndicho kiamue na si wananchi. Hata hivyo, kwa upande wa ukomo wa rais wamekubaliana iwe vipindi viwili vya miaka mitano, kama ilivyo sasa na rais huyo asiwe chini ya miaka 40. 
Mabadiliko mengine yaliyopendekezwa na kamati hiyo ni masuala ya gesi na mafuta yasiwepo kwenye Muungano. Suala hilo limeleta sintofahamu kubwa kati ya Zanzibar na Tanzania Bara, kwa sababu kwa sasa suala la gesi si la Muungano, lakini mafuta ni la Muungano. 
Akizungumzia uraia pacha, alisema lilileta mjadala mkali na pamoja na kupata elimu kutoka kwa wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Idara ya Uhamiaji. Alisema wameamua suala hilo waliache na kupigiwa kura bungeni, kwani waliona kiuchumi itasaidia uwekezaji nchini na watakaopewa uraia huo, wawe wenye utaalamu wa teknolojia kwa faida ya nchi. 
Wamekubaliana pia uhuru wa waandishi wa habari ulindwe, lakini waandishi walinde maadili ya fani hiyo. 
Kuhusu kero za Muungano zilizotajwa na rasimu ya Tume alifafanua: “Tumeona ina upungufu mkubwa, kuna kero na Warioba kasema za kikatiba, lakini kwa kushirikiana na Waziri
wa Fedha wa Zanzibar (Omar Yusuf Mzee) aliyepo kwenye kamati yetu, tumeona si sawa ni kero tu za kiutawala.
Mwenyekiti huyo alisema wajumbe wa Kamati yake, wameonesha nidhamu ya kuhudhuria vikao na wakati wote theluthi tatu ya wajumbe ilipatikana. Alisema Katiba inatakiwa kuandaliwa bungeni na si kwenye mikutano ya hadhara. Aliwataka wajumbe wa kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ambao wamesusa vikao hivyo, kurejea bungeni kwani nafasi hiyo upinzani waliililia muda mrefu sasa imepatikana. 
Alisema kinachotakiwa ni kuweka mbele suala la usalama wa Taifa, kuboresha Muungano na kukabiliana na maadui wa nchi waliopo sasa, ambao ni pamoja na udini na ukabila. 
“Mambo yote ya Tanganyika yaliingizwa mwaka 1964 kwenye Muungano, hivyo kwa Zanzibar ni sawa kuzungumzia mambo ya Zanzibar na ya Tanganyika, kwani ya kwao hayamo kwenyeMuungano na ya Bara ni sawa wao ni Watanzania.
“Ifahamike asilimia 60 ya Wazanzibari wametokea Bara, asilimia 95 ya Baraza la Mapinduzi la kwanza wametokea Bara kina Bavuai na wengine na Wazanzibari 500,000 wanaishi Bara. 
“Lakini sasa tumesahau hilo, tumegeuza siasa badala kuzungumzia kuimarisha Muungano, ifahamike Zanzibar ni njia  hivyo kuna umuhimu wake kwani biashara, uislamu, ukristo na ustaarabu vyote vilianzia Zanzibar, hivyo lazima kulindwe na kuangaliwe kipekee,” alisema.
Alihoji kama kusema Zanzibar kupepea bendera yake ni hoja, mbona kila jimbo Marekani linapepea bendera? “Tuangalie kwenye usalama wa nchi,” alisisitiza.

No comments: