VIPODOZI VILIVYOPIGWA MARUFUKU VYAUZWA DAR

Licha ya Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) kupiga marufuku vipodozi vyenye viambata vya sumu, vimeendelea kuuzwa katika masoko yaliyopo jijini hapa huku vingine vikiisha muda wake.
Utafiti uliofanywa na gazeti hili jana, umebaini kuwa baadhi ya vipodozi vilivyoko sokoni, vimepigwa marufuku kutumiwa na hata kuuzwa. 
Baadhi ya vipodozi hivyo ni  jaribu, betasol, lemovante, neuclear cream ambazo zote zimeisha muda wa matumizi, mecaco, zoa zoa na caro light ambavyo vipo katika masoko na watumiaji wananunua kutokana na kuuzwa bei ya chini. 
Ofisa Habari wa TFDA, Gaudencia Sinzamwa aliliambia gazeti hili kuwa vipodozi hivyo vimekuwa vikiingizwa kwa njia ya panya huku mamlaka hiyo ikikabiliana na waingizaji hao. 
Sinzamwa alisema wauzaji hao wanapitisha vipodozi hivyo kwa njia ambazo haziruhusiwi kwa kuwa wanatambua kuwa vipodozi hivyo vimepigwa marufuku kuuzwa katika jamii.
‘’Madhara yatokanayo na vipodozi hivyo ni saratani magonjwa ya ngozi, watumiaji wanashawishika kununua kutokana na bei nafuu, pia hawajali afya zao kwani elimu juu ya matumizi ya vipodozi tumeshatoa,’’ alisema Sinzamwa. 
Aidha alisema kwa kutumia fursa ya maonesho ya wakulima ya Nanenane yanatoa nafasi kwa watumiaji wa vipodozi hivyo kwa Mkoa wa Lindi na kwingineko kupata elimu zaidi kuhusu matumizi sahihi ya vipodozi.

No comments: