URAIA PACHA WAPASUA VICHWA VYA WAJUMBE

Suala la uraia wa nchi mbili, linaonekana kupasua vichwa vya wanakamati hasa wanaotoka Zanzibar, kutokana na historia ya nchi hiyo.
Kutokana na unyeti wa suala hilo imeelezwa na Katibu wa Bunge Maalumu la Katiba, Yahya Khamis Hamad, kuwa Bunge liliruhusu mtaalamu mwakilishi wa watu waishio nje, Kadiri Singo kuwasilisha waraka ambao umejadiliwa na kamati hizo.
Akifafanua zaidi taarifa zilizoenea kwamba kulikuwa na majadiliano makali kwenye ibara inayohusu masuala ya uraia wa nchi mbili, Hamad alisema pamoja na majadiliano hayo raia walioko nje ya nchi walituma waraka maalumu ambao waliomba ujadiliwe.
 “Juzi walimtuma mtaalamu wao, Singo alete waraka huo na niliomba kibali kwa mwenyekiti waraka huo uruhusiwe kujadiliwa ndani ya kamati na alipata ruhusa hiyo,’’ alisema Katibu.
Alisema hadi juzi mchana kamati tatu zilikuwa zikiendelea kujadili ibara inayohusu uraia pacha na kamati nyingine zimekamilisha kujadili ibara hiyo.
Naye mwenyekiti wa kamati namba 12, Paul Kimiti alisema kamati yake imekuwa ikijadili suala hilo la uraia pacha kwa kina, lakini kumekuwa na mvutano hasa kwa upande wa Zanzibar ambapo baadhi ya wajumbe wamekuwa na hisia tofauti kuhusu
uraia pacha kwa upande wao.
Kimiti alisema baadhi ya wajumbe wameonesha hofu kufuatia baadhi ya watu ambao walitoroka nje ya nchi wakati wa mapinduzi ambao wanaona kuruhusu uraia pacha kunaweza kuleta matatizo. Lakini wajumbe walikubaliana kuwa uraia pacha kwa waliotoroka nje wakati wa mapinduzi unaweza kudhibitiwa katika sheria itakayotungwa.
Kwa maoni yake Kimiti alisema inaonesha kuwa sura zilizokuwa zikileta mgogoro ni zilizohusu muundo wa serikali kwani kwa sasa wamekuwa wakiendelea bila tatizo.
Wakati huo huo, imeelezwa kuwa majadiliano yanayoendelea kuimarika zaidi
kutokana na kuzidi kuwasili kwa wabunge walikuwa wamesusia Bunge hilo. Pamoja na kutojulikana idadi ya waliorejea, Katibu alisema kundi la wajumbe 201 waliosusia wanaendelea kurejea bungeni na kuendelea na majadiliano ya kamati kama kawaida.

No comments: