UJENZI KITUO CHA VIWANDA, BIASHARA KURASINI KUANZAUjenzi wa mradi wa kituo kikubwa cha viwanda na biashara katika eneo la Kurasini jijini Dar es Salaam unatarajiwa kuanza hivi karibuni.
Matarajio hayo yanatokana na serikali kutenga Sh bilioni 53 zitakazotumika kuwalipa fidia wakazi wa eneo hilo kupisha ujenzi wa kituo hicho kijulikanacho kama Tanzania China Logistics.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Abdallah Kigoda aliwaambia waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam kwamba serikali imeshaipatia Mamlaka ya Ukanda Maalumu ya Uwekezaji (EPZA) mchakato wa ulipaji uanze mara moja kabla ya ujenzi kuanza.
Katika mradi huo, serikali ya China itawakilishwa na kampuni ya Yiwu Pan-Africa International Investment Corporation na Tanzania itawakilishwa na EPZA. Zaidi ya wananchi 1,020 wanatakiwa kuhama  eneo hilo la mradi.
Ujenzi wa mradi huo utagharimu Dola za Marekani milioni 400 ambazo ni sawa na Sh bilioni 660 ambazo zitagharimiwa na serikali ya China. Tanzania imetoa ardhi na kulipa fidia kwa wakazi wa maeneo hayo.
Eneo la mradi huu lenye ukubwa wa ekari 60.4 limetengwa katika kata ya Kurasini jijini hapa na linahusisha mitaa ya Shimo la Udongo, Mivinjeni na Kiungani. “Tunatarajia kituo hicho kuwa kikubwa Afrika ya Mashariki na Kati,” alisema Waziri.

No comments: