HIVI NDIVYO TRAFIKI FEKI ALIVYOTIWA MBARONI DAR

Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam  inamshikilia na kumhoji Robson Mwakyusa (30), mkazi wa Kijitonyama kwa tuhuma za kujifanya Ofisa wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani.
Mtuhumiwa huyo alikamatwa juzi maeneo ya Chamazi wilayani  Temeke, akiendelea na kazi ya ukaguzi wa makosa ya usalama barabarani, huku akiwa amevalia sare za Polisi na cheo cha Stesheni Sajenti.
Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova  alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa akiwa na gari lenye namba za usajili     T 723 BAK aina ya Toyota Cresta, yenye rangi nyeupe.
Kova alidai kuwa gari hilo, alikuwa akilitumia kuzunguka maeneo mbalimbali ya jiji , akiwadanganya kuwa yeye ni askari Polisi.
Alisema gari hilo lilipopekuliwa, lilikutwa na 'Radio Call' yenye namba GP380 aina ya Motorola leseni za udereva 40 za watu mbalimbali na 'Police Loss Report' mbalimbali.
Pia, alikutwa na kofia moja ya Usalama barabarani, beji yenye jina la E.R. MWAKYUSA ya kuweka kifuani, ratiba ya mabasi yaendayo mikoani ya SUMATRA na stakabadhi mbili
za Serikali zenye namba A0531562 na A1672464.
Kova alisema mtuhumiwa huyo alipopekuliwa nyumbani kwake, alikutwa na jozi nne za sare ya polisi za rangi ya kaki, jozi tatu za sare ya polisi Usalama barabarani, kofia na koti la mvua la usalama barabarani.
Pia, mtuhumiwa alikutwa na  'reflector' nane za Usalama barabarani, kofia mbili (barret) nyeusi za polisi, mikanda ya bendera mali ya jeshi la polisi, mikanda miwili ya polisi, mikanda miwili ya filimbi na cheo cha sajenti.
Mtuhumiwa huyo, pia alikutwa na vyeo vitatu vya Stesheni Sajenti, vifungo nane vya chuma mali ya jeshi la polisi, cheo kimoja cha Stesheni Sajenti cha JWTZ, fomu nne za PF3 na fomu 62 za 'notification' zilizojazwa.
Kova alisema mtuhumiwa huyo, aliwahi kuwa askari polisi aliyejiunga na jeshi hilo mwaka 2000 akiwa mwenye namba F2460. Lakini, alifukuzwa kazi kwa fedheha Machi 21 mwaka huu huko Kibaha mkoani Pwani, akiwa na cheo cha Stesheni Sajenti.
Alisema kilichokuwa kinashangaza, mtuhumiwa huyo alikuwa hapeleki mtu kituoni, bali alikuwa anamalizana nao na alikamatwa baada ya kutiliwa shaka na wananchi.
Alisema ameamua kumuonesha mtuhumiwa huyo hadharani ili wananchi wamtambue. Alisema wataendesha msako mkali ili kuwakamata watu wenye tabia kama hiyo.

No comments: