TAS YAOMBA ULINZI ZAIDI KWA MAALBINO



Katibu Mkuu wa Chama cha Maalbino (TAS), Zakia  Nsemo ameiomba Serikali iongeze ulinzi kwa watu wenye ulemavu wa ngozi kutokana na maisha yao kuwa hatarini.
Nsemo aliyasema hayo wakati akizungumza jijini Dar es Salaam juu ya vitendo vya kinyama vilivyoripotiwa kufanyiwa watu wenye ulemavu wa ngozi mkoani Tabora na Simiyu ambako watu wasiojulikana waliwakata baadhi ya viungo vyao na kutokomea navyo na mwingine kuuawa.
Alisema vitendo hivyo vimeanza kushika kasi tena kama ilivyokuwa kipindi kilichopita hali inayowafanya albino washindwe kufanya shughuli zao zinazowapatia riziki huku watoto wenye ulemavu wa ngozi pia wakishindwa kwenda shule.
Hivi karibuni  Susan Mungi (35) ambaye ni albino mkazi wa kijiji cha Buhelele kata ya Nsimbo wilayani Igunga, alikatwa kiwiko cha mkono wake na wahusika kutoweka nacho.
Katika tukio hilo, mume wa Suzan, Mapambo Mashili aliuawa kikatili kwa kupigwa na kitu chenye ncha kali kifuani na kichwani wakati akijaribu kumnusuru mkewe asikatwe mkono wake.
Tukio hilo limekuwepo wiki moja baada ya mtoto Upendo Sengerema (15) mkazi wa kijiji cha Usinge kata ya Uganza wilayani Kaliua mkoani Tabora kukatwa mkono na wahalifu ambao walikimbia.

No comments: