TANESCO YATAMBULISHA KIFAA KIPYA CHA UMEME


Shirika la Ugavi wa Umeme (Tanesco) mkoani hapa limetambulisha kifaa kipya ambacho ni mbadala wa kutandaza nyaya za umeme kwa maandalizi ya kupata umeme wa shirika hilo kwa wafugaji wa kuku pamoja na wananchi wanaojenga chumba kimoja ama viwili.
Kifaa hicho mbadala tayari nyaya zimesukwa ndani yake na kinajulikana kwa jina la
Readboard (Umeta) kinauzwa na shirika hilo kinatoa unafuu wa gharama ya kutandaza nyaya kwenye nyumba na badala yake unatumia kifaa hicho.
Katika mahojiano na gazeti hili kwenye Maonesho ya Wakulima kwenye Uwanja wa
Nyamhong’olo, nje kidogo ya Jiji la Mwanza, Ofisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja
mkoani hapa, Flaviana Moshi alisema kifaa hicho cha Umeta ni mbadala wa maandalizi ya kupokea umeme kutoka kwenye nguzo za umeme  badala ya kutandaza nyaya.
Akifafanua alisema badala ya kutandaza nyaya ili upokee umeme kutoka kwenye nguzo wamemrahisishia mwananchi kwa kifaa hicho cha Umeta ambacho kimeishasukwa kabisa tayari kwa matumizi ya umeme mkubwa na mdogo.
“Tanesco inafanya jitihada za makusudi ili kuhakikisha wananchi wote wanafikiwa na
huduma hii kila sehemu ili waweze kukuza kipato chao kutokana na nishati ya umeme,” alisema Moshi.
Alisema kuwa Umeta ni kwa ajili ya wale ambao wamejega chumba kimoja, kwa matumizi ya kawaida au ya kufugia kuku, baada ya kulipia gharama kisha mafundi wa Tanesco hufika nyumbani kwa mteja kwa ajili ya kuweka na kutoa elimu ya namna ya kukitumia.
Moshi alisema kuwa tofauti na kuwasha  taa za ndani tu,  kifaa hicho kinatumika pia kuwashia jokofu, kupikia na kuangalia televisheni.
Alisema hii ni mara ya kwanza kwa Tanesco kushiriki Maonesho ya Wakulima ambapo
alisema  kuwa wamekuwa na manufaa sana kutokana wafugaji wengi kujitokeza na kupata maelekezo juu ya kifaa cha Umeta.

No comments: