SWALA OIL KUJIORODHESHA DSE KESHOKUTWA

Kampuni ya Swala Oil & Gas inayojihusisha na masuala ya uchimbaji wa mafuta na gesi, itajiorodhesha rasmi katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) keshokutwa. 
Hatua hiyo inatokana na kukamilika vizuri kwa ofa ya awali kwa umma, ijulikanayo kwa kifupi kama IPO baada ya kukamilika ofa ambayo ilianza Juni 9, 2014 hadi Julai 4, 2014. 
Kampuni hiyo ya Swala ilitarajia kuuza hisa milioni 9.6 za kawaida. Lakini, waliuza hisa zaidi ya lengo na kufikia milioni 13.3 na kwa sasa ina wanahisa wapya 1,868. 
“Utaratibu wa ofa za awali kwa umma, umekamiliki vizuri na ofa za awali za Swala zilizidi idadi iliyokusudiwa kujiunga na kwa wale ambao hawakuweza kununua hisa za Swala katika mgawo wa awali, wataweza kuzinunua katika soko la hisa katika siku hizo zilizotajwa,” alisema Meneja Mratibu wa DSE, Magabe Maasa. 
Alisema Kampuni ya Swala itakuwa  ya 20 kuorodheshwa DSE. Pia, itakuwa kampuni ya kwanza ya mafuta na gesi kuorodheshwa katika soko la hisa ndani ya Afrika Mashariki. 
Meneja Mkuu wa Swala, David Mestres aliongeza, “Tunafurahi sana kuongezeka kwa waliojiunga,  hali hii inaonesha ari iliyopo Tanzania ya kuwekeza katika maliasili”. 
Alisema mwamko huo unaonesha maendeleo ambayo DSE imekuwa ikijitahidi kuwashawishi wawekezaji wa ndani na nje ya nchi katika biashara za Tanzania. 
Swala ni kampuni ya kwanza ya  mafuta na gesi katika orodha ya soko la hisa la Afrika Mashariki. Ipo chini ya kivuli cha Swala Energy Limited,  kampuni  ambayo iko kwenye orodha ya soko la hisa la Australia (ASX), ikijulikana kwa kifupi kama SWE.

No comments: