SUMAYE ATAJA SIFA ZA VIONGOZI WAZURI

Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye amesema Watanzania wanatamani kupata viongozi wazuri na wanamwomba Mungu awasikilize na awasaidie katika hilo, huku akitaja baadhi ya sifa ambazo wangependa viongozi wao wawe nazo. 
Aidha, amesema Tanzania hivi sasa inapita katika wakati wenye changamoto nyingi  na wakati huu kuna mambo makubwa na mazito, ambayo yanahitaji kuombewa kwa Mungu, ambayo ni amani na utulivu na kupata viongozi wazuri.
Sumaye alisema hayo jana kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam wakati alipokuwa akizungumza kwenye uzinduzi wa albamu ya Kamata Pindo la Yesu ya mwanamuziki nyota wa injili nchini, Rose Muhando.
Alitaja sifa ambazo  Watanzania wanatamani viongozi wao wawe nazo kuwa ni kutambua na kuthamini umoja, kiongozi bora anayejiamini, uadilifu, kupiga vita rushwa na maovu mengine kama ufisadi, matumizi ya dawa za kulevya, mauaji, ujambazi na mengineyo, kupiga vita umasikini
Sifa nyingine ni kuboresha huduma za jamii, nidhamu na utendaji kazi, kusimamia mapato na matumizi ya fedha za umma, kukuza uchumi imara na mzalendo.
“Tunahitaji kuwa na amani na utulivu wakati wa uandikishaji wa wapiga kura katika daftari la wapiga kura, wakati wa kampeni zetu, wakati wa upigaji kura na hatimaye wakati wa kutangaza matokeo. Maeneo haya manne ni muhinmu sana yakatekelezwa kwa umakini na kwa haki na uwazi kadri inavyowezekana,” alisema Sumaye aliyedumu katika nafasi yake kwa miaka 10.
Aidha, alisema wakati wa mchakato mzima wa uchaguzi kuanzia uandikishaji, wakati wa kampeni, upigaji kura, kuhesabu kura na kutangaza matokeo na kukubali matokeo, ni lazima kila mhusika ahakikishe anatimiza wajibu wake ili kutoleta vurugu na kuharibu amani ya nchi.
Kuhusu kupata viongozi wazuri,  Sumaye alisema: “Hivi sasa taifa letu linapita kwenye mchakato wa Katiba mpya, ni vema kuhakikisha kuwa mchakato huu hautupeleki kwenye kudhoofisha Muungano wetu na mshikamano wetu kama taifa.
“Watanzania tumekaa kwenye Muungano wetu kwa miaka 50 sasa kwa amani na mshikamano na hatutarajii kiongozi atakayetuingiza katika majaribio. Tuna mafunzo ya kutosha kwa baadhi ya nchi ambazo zimejigawanya jinsi ambavyo zimepoteza amani waliyokuwa nayo.”
Aliongeza: “Hizi ni baadhi tu ya sifa ambazo Watanzania wa wangependa kiongozi wao awe nazo. Katika sala zao wanapomwomba Mungu kila moja kwa namna yake wanatamani Mungu awapatie kiongozi wa sifa hizo na zingine nzuri ambazo mimi sikuzitaja. Wakina Rose Muhando na wenzake ndiyo sala zao na sisi ndiyo sala zetu.”
Sumaye alisema pamoja na kumwomba Mungu atuvushe salama kama taifa, kama vyama vya siasa na kama mtu mmoja mmoja, lazima tutekeleze wajibu wetu.
“Hatuwezi kumwomba Mungu atuvushe salama huku sisi wenyewe kwa makusudi tunakoroga misingi ya amani na utulivu wetu,” alisema.

No comments: