STAMICO YATOA SHILINGI MILIONI 800 KWA MAENEO YA MGODI BUHEMBA

Serikali kupitia Shirika  la  Madini la Taifa (Stamico) limetoa  takribani Sh milioni 800 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa, nyumba ya mwalimu na kituo cha afya katika eneo la mgodi wa Buhemba  ulioko Musoma, mkoani Mara.
Ujenzi huo ni sehemu ya uwajibikaji kwa jamii, hususani kwa mwekezaji anayefanya  shughuli  katika migodi.
Kadhalika wachimbaji wadogo wa maeneo hayo, waliopo katika vyama vya ushirika, wamepewa hekta zaidi ya tisa kama viwanja vya madini kwa ajili ya uchimbaji mdogomdogo.
Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Angelina Mabula alitoa ushuhuda wa ujenzi huo, jijini Dar es Salaam jana mbele ya Kaimu Mkurugenzi  Mtendaji wa Stamico, Edwin Ngonyani pamoja na watendaji wengine wa shirika hilo.
Mabula alisema awali mgodi huo ulikuwa na migogoro mbalimbali kutoka kwa jamii iliyouzunguka  pamoja na wachimbaji wadogo juu ya uwajibikaji kwa jamii, lakini kwa sasa kumetulia na wanaishuruku serikali kuwekeza kupitia shirika hilo.
Kuhusu ujenzi wa vyumba vya madarasa alisema vitajengwa vyumba vitatu katika shule ya Biatika pamoja na nyumba ya mwalimu, huku kituo cha afya kikijengwa eneo la Buhemba na vyumba vingine vitatu vya madarasa kujengwa shule ya Kamenga.
“Mradi wa ujenzi huo  ni wa miezi minne ukianzia Julai mwaka huu…pia vijana 20 wamepelekwa kusomea chuo cha madini kilichopo mkoani Dodoma na wengine 50 katika vyuo vya ufundi stadi (Veta) kuwezesha upatikanaji  wa ajira kutoka kwa jamii inayouzunguka mgodi,” alisema Mabula.
Kuhusu wananchi waliopewa viwanja vya madini alisema ni wale waliopo katika vyama vya ushirika vya Buhemba Miners Cooperative Society, Tugeme, Mirwa na Mwangaza Miners cooperative society  jambo lililosababisha jamii inayouzunguka mgodi huo kutulia.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Stamico, Ngonyani alisema shirika hilo limepewa jukumu la kuwekeza hivyo wakiwa kama wawekezaji wanategemea kuchangia katika  jamii.
“Wapo wanaodhani kuwa shirika hilo haliwezi kufanya hivyo waelewe kuwa Stamico ni shirika kama walivyo wengine,” alisema Ngonyani na kusema pia katika mgodi huo lina maeneo mawili ya utafiti, uchimbaji na uchenjuaji.

No comments: