SHERIA YATUNGWA KUDHIBITI ULAFI WA VIONGOZI



Mapendekezo ya Sheria ya Mgongano wa Maslahi miongoni mwa viongozi na watumishi wa umma, kutenganisha viongozi, mali na biashara zao, ili kuzuia ukiukwaji wa maadili ya viongozi wa umma unaoendelea kutokea nchini yamewekwa hadharani.
Katika mapendekezo hayo yaliyowasilishwa jana Dar es Salaam na mtoa mada kutoka Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Gertrude Cyriacus, pamoja na mambo mengine, viongozi wote wa umma na watumishi wa umma, watatakiwa kuchagua kati ya mali na biashara zao na nafasi ya utumishi wa umma.
Uchaguzi huo utafanyika kwa namna mbili; moja kukabidhi biashara zote kwa kampuni ya udhamini, ambayo itaendesha biashara hizo huku mtumishi mwenye mali, akinyimwa taarifa muhimu za biashara yake.
Pili mali na biashara ambazo kiongozi wa umma atakuwa nazo, ambazo zinaweza kusababisha mgongano wa maslahi, atatakiwa kuziuza kabla ya kukubali kazi ya kutumikia umma au kampuni ya udhamini, inaweza kuuza mali hizo bila hata kumpa taarifa.
Kwa mujibu wa mapendekezo hayo,  kiongozi  wa umma atatakiwa na sheria kuweka mali zake katika kampuni hizo za udhamini, ambazo zitateuliwa na kupewa masharti ya kuendesha biashara za viongozi.
Sheria hiyo itatamka viongozi watakaohusika kuweka mali au biashara zao kwenye kampuni hizo, ambao watakuwa viongozi wote wa kisiasa na viongozi waandamizi.
Pia mapendekezo ya sheria hiyo yameweka wazi aina za biashara ambazo Kiongozi wa Umma, atatakiwa kukabidhi kwenye kampuni hizo, ambapo pia kiongozi husika hatokuwa na madaraka yoyote kuhusu uendeshaji wa biashara zake zitakazosimamiwa.
“Kampuni za udhamini hazitatoa taarifa yoyote kwa kiongozi husika kuhusu biashara zake, isipokuwa tu taarifa kuhusu thamani ya biashara husika,” alisema Gertrude wakati akiwasilisha mapendekezo hayo.
Aidha, mapendekezo ya sheria hiyo yametamka muda wa mwaka mmoja kwa ajili ya Kiongozi wa Umma kupata taarifa kuhusu kodi ya mapato na thamani ya biashara alizoziweka katika kampuni za udhamini na taarifa hiyo itapitia kwanza katika Sekretarieti ya Maadili.  
Kwa masharti hayo, kwa mujibu wa mapendekezo ya sheria hiyo, kampuni za udhamini, zitatakiwa kuwasilisha taarifa za mali na shughuli za biashara kila mwisho wa mwaka, kwa Kamishna wa Maadili kwa utaratibu utakaowekwa.
“Kampuni za udhamini zitakabidhi mali na biashara mara Kiongozi wa Umma atapohitimisha muda wake wa uongozi. Aidha, kampuni ya udhamini haitawajibika na hasara yoyote itakayotokea katika biashara husika, ili mradi  ifanye kazi yake kwa nia njema na kwa kufanya uamuzi wa busara,” imeelezwa katika mapendekezo hayo.
Ingawa kampuni hizo za udhamini, zitakuwa na kinga, ikiwa biashara ya kiongozi itapata hasara, pia kampuni hizo zimepewa mamlaka  ya kuuza mali ambazo   zinaweza kumsababishia Kiongozi wa Umma kuingia katika  mgongano wa maslahi.
Mbali na uwezo huo wa kuuza mali, viongozi pia wamewekewa zuio wasitoe maagizo kwa  kampuni ya udhamini,  itakayoteuliwa kusimamia biashara husika.
“Sheria imtake kiongozi wa umma ambaye hataridhia kuweka mali zake kwenye kampuni za udhamini, kuchagua kuuza mali ambazo  zinaonekana zinaweza kumuingiza kwenye mgongano wa maslahi,” imeelezwa.
Sheria hiyo pia itazuia viongozi wa umma walioko madarakani, kujiongezea maslahi ya aina yoyote na kama wakifanya hivyo, maboresho hayo ya maslahi, hayatatekelezwa mpaka atakapoondoka katika cheo husika.
“Sheria iweke masharti yatakayozuia kiongozi kushiriki kufanya uamuzi wa uboreshaji wa maslahi, yanayohusu nafasi anayoitumikia na maboresho yoyote yatakayofanyika, yaanze kutumika baada ya kiongozi husika kuondoka katika wadhifa husika,” imeelezwa.
Lengo la kipengele hicho, limetajwa kuwa ni kumfanya kiongozi atekeleze majukumu kwa misingi ya haki, usawa na uaminifu kwa kuwa, Sekretarieti ya Utumishi wa Umma, imebaini kuwa baadhi ya viongozi wenye dhamana ya kusimamia taasisi za kuboresha maslahi, hutumia fursa hiyo kujinufaisha binafsi kwa kuboresha maslahi kwa kipindi wanachokuwa madarakani.
Kuhusu zawadi, Sheria hiyo inatarajiwa kuzuia watumishi wa umma kutoa zawadi kwa wasimamizi wao wa kazi.
Lengo la zuio hilo, ni kuondoa uwezekano wa kuathiri uamuzi kwa misingi ya haki na usawa, kwa kuwa imebainika kuwa baadhi ya zawadi ni rushwa ya kuwekeza, inayotolewa kwa malengo ya kujinufaisha baadaye.
Akizungumza katika semina hiyo, mgeni rasmi, Rais wa Awamu ya Tatu,  Ali Hassan Mwinyi, alisema Serikali haijawahi kufuta Azimio la Arusha kama inavyodaiwa na baadhi ya wananchi, bali ilizimua azimio
hilo kuwapatia viongozi wa kati, uwezo wa kumudu makali ya maisha.
Lengo la kipato hicho kwa mujibu wa Mzee Mwinyi,  ilikuwa kuwasaidia  kumudu mahitaji ya maisha na kupata haki ya kikatiba ya uhuru wa kuwa na mali ya akiba ndogo, ili imuokoe mtumishi wakati wa dharura kama vile kuugua au kufiwa.
“Ninyi ni mashahidi kuwa hali hiyo ilikuwa kinyume cha matarajio, kwani watu wamekuwa wakitumia vibaya haki ile ya kikatiba, kwa kumiliki mali hata kwa njia zisizo halali…  tuliwaruhusu kuingiza mkono, lakini wao wakaingiza mwili mzima,” alisema.
Kamishna wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Jaji Salome Kaganda, alisema makusudi ya mapendekezo ya sheria hiyo ni kuleta amani na utulivu wa nchi.
“Mapendekezo ya sheria hii, hayalengi kuwafanya viongozi kuwa maskini, bali kasi yao ya ukwasi iendane na hali halisi ya kipato chao.
 “Lazima kuwepo na hatua ya Serikali kurejesha maadili ya  viongozi, kama itazingatiwa na kuheshimiwa, Taifa litafikia maendeleo ya haraka yaliyokusudiwa,” alisema Jaji Kaganda.

No comments: