SHEIN ASEMA Z'BAR INAWATHAMINI WAISHIO UGHAIBUNI

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), imesema inathamini mafanikio makubwa yaliyoanza kupatikana kutoka kwa Wazanzibari wanaoishi nchi za nje (Diaspora) na ndio maana ina mpango maalumu wa kuandaa Sera na hatimaye Sheria kwa lengo la kuendeleza zaidi mafanikio hayo.
Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein aliyasema hayo jana baada ya chakula maalumu cha mchana alichowandalia Wazanzibari wanaoishi nchi za nje (Diaspora) huko katika viwanja vya Ikulu, mjini hapa.
Katika hafla hiyo iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwamo Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi, Spika wa Baraza la Wawakilishi, Mawaziri, Wawakilishi, Wabunge, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Abdalla Mwinyi Khamis, Makatibu Wakuu na viongozi wengine.
Wazanzibari wanaoishi nchi za nje  waliojumuika katika hafla hiyo iliyoandaliwa na  Dk Shein ambao wapo hapa nchini kwa mapumziko ni kutoka  nchi mbalimbali zikiwamo Uingereza, Canada, Marekani, Denmark, Sweden, Oman, Falme za Kiarabu, Ujerumani, Uholanzi, Austria na Uswisi.
Akitoa nasaha zake, Dk Shein alisema michango na misaada yao imeanza kitambo kwa kusaidia nyenzo na vifaa mbalimbali hapa nchini na kuzitaja nchi kadhaa ambazo tayari zimeshapata mafanikio kutoka kwa wananchi wake waishio  nchi za nje.
Alisema mbali ya vifaa na nyenzo hizo, Wanadiaspora hao pia wamechangia utaalamu walionao ikiwa ni pamoja na kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuendeleza sekta ya elimu Zanzibar kupitia Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) kwa kuweza kufundisha elimu ya Shahada ya Uzamivu.
Dk Shein alieleza kuwa wataalamu hao wameweza kutoa utaalamu wao kwa Shahada hiyo ya Uzamivu katika lugha ya Kiswahili na tayari hivi sasa wanafunzi wanaowafundisha wanaendelea na masomo yao vizuri na pia wapo wengine waliojitokeza kuonesha uzoefu wao wa kazi.
Alisisitiza kuwa nia na lengo la Serikali ni kufanya vizuri zaidi kwani ishara ya mafanikio imeshajitokeza kwa hivi sasa na kusisitiza kuwa kila Mzanzibari alieko nje na ndani ya Zanzibar ana fursa na nafasi ya kuijenga nchi yake.
Pia alieleza kuwa mchakato huo wa kuanzisha Diaspora wa Tanzania wakiwemo kutoka Zanzibar aliuanza yeye na Rais Jakaya Kikwete tangu yeye akiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutambua umuhimu wake.
Aidha, Dk Shein aliwataka Wanadiaspora kuendeleza misingi ya amani na utulivu kwani ni kawaida ya Wazanzibari wakiishi nchi za nje huwa hawabadilishi hulka wala desturi zao hatua ambayo imewajengea sifa kubwa. “Zanzibar inasifika sana kwa amani na utulivu,” alisema Dk Shein.

No comments: