RAIS KIKWETE AAMINI KATIBA MPYA ITAPATIKANA

Wakati Bunge Maalumu la Katiba likitarajiwa kuanza leo, huku mjadala mkali kuhusu mchakato wa Katiba mpya ukiendelea katika makongamano mbali mbali, Rais Jakaya Kikwete amesema ana matumaini baada ya mjadala na changamoto, Katiba mpya itapatikana.
Rais Kikwete alisema hayo Jumamosi iliyopita usiku mjini Washington, Marekani  alipokuwa akizungumza na   Watanzania wanaoishi katika nchi hiyo kutoka maeneo ya Jiji la Washington D.C na majimbo ya Virginia, Maryland, California na New York.
“Najua kuwa mchakato wa Katiba umekuwa na changamoto katika siku za karibuni, lakini kwangu mimi mchakato huo ni sawa na barabara ndefu ambayo haikosi kona. Kona zitakuwepo lakini mimi ni mtu ambaye naishi kwa matumaini na ni matumaini yangu kuwa mchakato huo utaendelea na hatimaye kufikia mwisho vizuri kama tunavyotarajia wote,” alisema Rais Kikwete.
Rais Kikwete pia alisema pamoja na changamoto za mchakato huo, Serikali haina wasiwasi na hali hiyo, kwa kuwa ndiyo hali ya uendeshaji wa nchi ya kidemokrasia.
“Najua kuwa maneno yamekuwa mengi, lakini si ndiyo demokrasia ya wazi inavyofanya kazi? Sisi katika Serikali hatuna wasiwasi na hali hiyo. Ndiyo mambo yanavyotakiwa kuwa katika nchi ambako demokrasia inafanya kazi,” alisema Rais Kikwete ambaye wiki iliyopita, alikabidhiwa Tuzo ya Kimataifa ya Nyota wa Demokrasia Afrika 2014.
Aliwaambia Watanzania hao, kuwa yale mambo yanayosumbua kwa sasa, ikiwemo hilo la Ukawa kususia Bunge Maalumu la Katiba, yanazungumzwa na vyama. Alieleza kuwa anaamini majawabu yatapatikana. 
Rais Kikwete alisema kuwa mchakato huo, kimsingi, unatakiwa kuongozwa na ukweli kuwa Katiba inahusu wananchi wenyewe na maisha yao, na wala siyo tu mchakato huo kuongozwa na mjadala wa idadi ya serikali mbili ama tatu.
“Mchakato wetu kwa muda mrefu, umekuwa kuhusu idadi ya serikali, ziwe mbili ama ziwe tatu. Kwangu mimi, idadi ya serikali ni muhimu, lakini naamini kuwa Katiba iwe ni kuhusu maisha yenyewe ya wananchi na ustawi wao, mwelekeo mzima wa mchakato huo usiwe kuhusu idadi ya serikali tu,” alisema.
Kwa mujibu wa Rais Kikwete, ni dhahiri kuwa yapo mengi ambayo hayajakaa sawasawa katika mchakato mzima, hasa kuhusu jinsi Katiba mpya itakavyolinda maisha ya wananchi na kusaidia kuboresha ustawi wao.
“Naamini kuwa yapo mengi kuhusu Katiba ambayo hayajapata muda wa kutosha wa kuyajadili katika Bunge Maalumu la Katiba. Kimsingi, Katiba ni Katiba ya wananchi, ni Katiba kuhusu maisha yao na ustawi wao. Hili jambo sijaona kama linaonekana sana katika mjadala wa Katiba,” alisema mshindi huyo wa Tuzo ya Kimataifa ya Nyota wa Demokrasia Afrika 2014.
Akizungumza katika Kongamano la Katiba lililofanyika Dar es Salaam jana, Mweyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji mstaafu Joseph Warioba alisisitiza mwito wake kwa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, kujadili na kukubaliana kwa maridhiano.
Alishauri wajumbe ambao wanakinzana, wapewe fursa ya kujifungia mahali, wajadili mpaka wapate maridhiano na kutoka katika hiyo sehemu wakiwa na muafaka.
Kwa mujibu wa Jaji Warioba, mchakato huo wa Katiba mpya, si lazima ukamilike mwaka ujao ili kuondoa hofu ya baadhi ya wajumbe wanaojadili huku wakijipanga namna ya kushinda Uchaguzi Mkuu ujao.
Badala yake, alishauri mjadala ufanyike taratibu na ukikamilika, kabla ya Katiba inayopendekezwa kupelekwa kwa wananchi kwa kura ya maoni, mambo machache muhimu kwa ajili ya uchaguzi mkuu, yachukuliwe kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu na Katiba inayoependekezwa, ipigiwe kura katika Awamu ya Tano ya Serikali. 
Akielezea uzoefu wa namna wajumbe wa Bunge hilo walivyotofautiana na kuishia kuwa wamoja, Warioba alisema: “tulichambua kazi tuliyopewa na kuelewa nini tumekabidhiwa na tunatakiwa kufanya, pamoja na tofauti zetu tulifikia kuelewana.
“Sasa hivi (wajumbe wa Bunge Maalumu) mnatofautiana juu muundo wa Serikali, itafika mahali mtakuwa pamoja mtafika mahali ya kuwa wamoja,” alisema Warioba, neno lililoashiria ana matumaini kama ya Rais Kikwete.
Jaji Warioba alisema kuna wataalamu walikuja kusaidia Tume katika mchakato huo, na walipoiona Rasimu ya Katiba, walikuwa na shaka kama itapita, kwa sababu ilikuwa inagusa maslahi ya viongozi wanaokwenda kuipitisha.
“Sisi tukawaambia wananchi wamesisitiza mawaziri wasiwe wabunge na ukomo wa ubunge, mwananchi mmoja aliwahi kusema siku hizi hakuna uchaguzi bali ni minada,” alisema Jaji Warioba.
Alisema walijipa moyo na kuamini kuwa viongozi wa Tanzania, wana uzoefu wa kufanya uamuzi mgumu, ukiwemo wa Azimio la Arusha, ambalo viongozi walipitisha pamoja na kuwa wao nao walikuwa waathirika.
Baada ya kuelezea matumaini yake ya kufikia mwisho mwema kwa makubaliano baada ya kuhitilafiana,  Warioba alitaka wajumbe wa Ukawa kurudi bungeni kwenda kutafuta muafaka.
“Machali nendeni mkazungumze na kufikia maridhiano, kiongozi lazima ajiamini, lakini sasa kila mkitoa matamko basi ni kushambuliana, tafuteni lugha ya kujenga na mwongozo wenu uwe Taifa na si chama.
“Tukienda kwa mtindo wa vyama, tutapata matatizo, wabunge wanatakiwa kutafuta muafaka kwa maslahi ya Taifa,” alisema Warioba.
Mjumbe wa Tume hiyo, Joseph Butiku, alipokuwa akijibu swali kama hotuba ya Rais Kikwete ya ufunguzi wa Bunge Maalumu la Katiba, iliharibu mchakato huo, alisema Rais Kikwete asisingiziwe kwa kuwa ndiye aliyeruhusu mchakato wa Katiba ufanyike, kutokana na hali ya kisiasa ya wakati huu.
Alisema Rais Kikwete alitoa maoni kama Mtanzania na tume ina heshimu maoni hayo na sehemu iliyotumia kuyatoa.
" Yalikuwa ni maoni,  yapo maeneo alitoa kwa msisitizo, yapo maoni aliyotoa unaona yanakoelekea ya kutetea Chama Cha Mapinduzi (CCM).
“ Lakini mlioko bungeni, kila wakati alikuwa anasema 'ninyi tumie akili zenu kujadiliana kwa kina na kwa uwazi na mtoe uamuzi,'  kama wewe uliona alilosema si la kutumia, shauri yako,” alisema Butiku.
Butiku alisema mchakato wa Katiba, si wa vyama au kundi na kusisitiza kuwa ni wa wananchi na  ni wa kisheria, ambao ulilenga kukusanya maoni ya wananchi na si ya maaskofu, CCM au Ukawa na ilitoa nafasi kwa wananchi kushiriki kwa uwazi, uhuru na upana.
Alisema hakuna aliyekataa muundo wa Serikali mbili, lakini mfumo huo unatakiwa kufanyiwa ukarabati mkubwa, na kuhoji kama Zanzibar watakubali ukarabati huo, ambao ni kuondoa neno ‘nchi’ katika Katiba yao, kupitia kura ya maoni.

No comments: