RADI YAUA WANAFUNZI WAWILI NA KUJERUHI



Wanafunzi wawili wa Shule ya Sekondari Kamuli wilayani Kyerwa mkoani Kagera wamekufa na mmoja kujeruhiwa kwa kupigwa radi.
Makamu Mkuu wa shule hiyo, Marco Renatus alisema juzi saa 7 mchana radi ilipiga nyumba waliyokuwemo wanafunzi hao wakati mvua kubwa iliyoambatana na mawe na upepo mkali iliponyesha.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kagera, Henry Mwaibambe alithibitisha kuwepo tukio hilo.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi jana, Mwalimu Renatus alitaja wanafunzi waliopoteza maisha ni Amoni Aniseth (20)  wa Kidato cha Nne na Onesmo Odiro (14) wa  Kidato cha Kwanza.
Kwa mujibu wa mwalimu huyo, radi ilibomoa ukuta wa chumba cha kwanza na chumba cha pili, ambako wanafunzi hao walikuwa wamelala.
Amoni alipoteza maisha  baada ya kufikishwa katika kituo cha afya Kamuli wakati Odiro alifariki saa 5 usiku katika Hospital ya Isingiro wilayani Kyerwa.
Majeruhi, Filibath Jackisonali wa Kidato cha Tatu  aliruhusiwa jana baada ya kupatiwa matibabu na kuonekana afya yake inaendelea vizuri.
Mganga aliyekuwa zamu katika hospitali ya Isingiro, Letisia Masito alisema alimpokea Onesmo juzi saa 2 usiku na kwamba akiwa katika harakati za kumpatia matibabu saa 5 usiku, ndipo alipoteza maisha.
Hili ni tukio la pili la radi ndani ya wiki moja baada Agosti 14 mwaka huu, watu wawili katika kata ya Kanoni wilayani Karagwe, kupoteza  maisha kutokana na kupigwa radi.

No comments: