PROFESA SHIVJI AITWA KUSAIDIA BUNGE MAALUMU



Bunge Maalumu la Katiba, limemwalika Mhadhiri mashuhuri wa masuala ya Katiba, Profesa Issa Shivji, kuwasaidia aina ya Muungano na namna mambo yake yatakavyoingizwa kwenye Katiba.
Pia Bunge hilo limepokea mapendekezo ya nyongeza ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, yaliyokuwa yamehifadhiwa, ili yatumike wakati wa kuunda katiba ya Tanganyika, yajadiliwe na kamati hizo.
Uamuzi huo ulifikiwa jana kwenye Kamati ya Uongozi, iliyokaa ambapo Mwenyekiti wa Bunge, Samuel Sitta, aliunda Kamati Ndogo ya Kamati ya Uongozi, kufanyia kazi kwa undani mambo ambayo kamati nyingi zimeshindwa kufikia muafaka.
Mambo hayo ni pamoja na Mahakama ya Kadhi, Muundo wa Bunge na kuangalia mambo ya muungano, uraia pacha na Kamati ya Pamoja ya Fedha ya Muungano. 
Akizungumza na waandishi wa habari juu ya yaliyojiri kwenye Kamati hiyo ya Uongozi wakati wa kupitia tathmini ya mwenendo wa Bunge, Sitta alisema Bunge limeona limwalike Profesa Shivji kutokana na kuwa na maandiko mengi ya muundo wa Muungano.
Kwa matarajio ya Sitta, Profesa Shivji atasaidia aina ya Muungano unaofaa na mambo  yake yatazingatiwa wakati wa kutengeneza muundo huo.
Kamati hiyo ndogo aliyounda ina wajumbe kumi, watano kutoka Tanzania Bara na watano Zanzibar na itakuwa chini ya Makamu Mwenyekiti wa Bunge, Samia Suluhu Hassan na kwa kuanza alisema: “Nimeagiza wataalamu wa ngazi za juu waje kukutana na kamati ndogo kwa kina na kwa kamati ya fedha, watakuja makatibu wakuu na magavana kutoka Serikali ya Jamhuri na ya Mapinduzi na magavana hao, waje kabla ya Jumamosi (kesho kutwa)”. 
Kwa upande wa uraia pacha, alisema watakuja wataalamu kutoka Idara ya Uhamiaji akiwemo mhadhiri wa masuala ya uraia pacha ambapo wote, watatoa elimu zaidi kuwasaidia wajumbe kufikia muafaka wa masuala hayo. 
Mwenyekiti huyo wa Bunge Maalumu la Katiba alisema wamekubaliana kwenye Kamati ya Uongozi, kupeleka kwenye kamati 12 za Bunge, andiko la Tume ya Jaji Joseph Warioba, ili yazingatiwe wakati wa kuundwa kwa serikali ya Tanganyika.
Mambo hayo ni ardhi, mazingira na rasilimali za Taifa ambapo Sitta amesema wameyachukua bila kubagua aina ya serikali.
Alitaja mambo mengine waliyoyachukua na kuwasilishwa kwa Kamati ili yajadiliwe na kuongezwa kwenye rasimu hiyo, ni yaliyoletwa na Waziri wa Katiba na Sheria ya mapendekezo kutoka Jumuiya ya Serikali za Mitaa (ALAT) ya kutambuliwa Serikali za Mitaa kwenye Katiba.
Vilevile wameyaingiza mapendekezo ya kuwepo maeneo mahususi kama kuwa na sehemu ya kutosha kuelezea jukumu la serikali, katika kujenga uchumi imara  hivyo wameona kuanzishwe sura mpya ya Lengo la Maendeleo ya Kiuchumi.
Pia yamo mapendekezo ya haki za wachimbaji wadogo, wakulima na wavuvi. Pia haki za kuwalinda watumiaji bidhaa na haki za makaburi ambapo marehemu watapewa heshima, iliyowasilishwa na Yasmin Aloo. 
Sitta alisema kamati zote zinakwenda vizuri, ila tatizo ni baadhi ya wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano mahudhurio yao si mazuri kwa kuwa wanakwenda sana majimboni lakini wawakilishi kutoka Zanzibar mahudhurio yao ni mazuri.

No comments: