PINDA ACHARUKA, ATAKA MAJIBU YA UZEMBE NDANI YA SAA 30

Waziri Mkuu Mizengo Pinda ametoa saa 30 na kutaka kupatiwa majibu, ni kwa nini maelekezo aliyotoa kuhusu kiwanda cha kusindika nyama cha Mbeya, hayajafanyiwa kazi.
Alitoa kauli hiyo jana mchana wakati akizindua Kongamano la siku tatu la Uwekezaji la Mikoa ya Iringa, Njombe na Mbeya la mwaka 2014. Kongamano hilo lilianza kwenye ukumbi wa Benjamin Mkapa jijini Mbeya.
“Mbeya inaweza kuwa na fursa kubwa ya viwanda vya usindikaji nyama, unga wa mahindi ili kuongeza thamani ya mazao mnayozalisha katika mkoa wenu. Nilipokuwa hapa ziara yangu ya mwisho 2012, niliagiza kiwanda hiki kitafutiwe mwekezaji ili kianze uzalishaji. Jana nimeuliza kiwanda cha nyama kimefikia wapi, naambiwa watu bado wanaongea. Wanaongea nini?,” alihoji.
“Mtu akija kusikia habari ya kiwanda hiki, atatuona ni wajinga tena ni wajinga wa kujitakia, kisa watu bado wanazungumza…hiki kiwanda cha nyama ni cha Mbeya na manufaa yake ni kwa ajili ya wana Mbeya. Hivi wahusika kwani hamuioni hiyo fursa?” alisema.
“Dk Mary Nagu watafute watu wa CHC, waje hapa kujieleza ni kwa nini suala hili limechukua muda mrefu. Kabla sijaondoka hapa Mbeya kesho (leo) nataka nipate majibu kuhusu jambo hili,” aliagiza.
Katika hotuba yake ya ufunguzi, Waziri Mkuu alisisitiza suala la watendaji wa mikoa na wilaya, kuchukulia kwa umakini suala la uwekezaji, kwani wasipofanya hivyo wao ndiyo watageuka kikwazo na kukwamisha maendeleo ya wananchi wanaowaongoza.
“Ndugu zangu wa Serikali za mitaa msiwe vikwazo, kuweni wawezeshaji. Ninyi si watawala, bali ni waleta maendeleo kwa jamii. Natoa wito mshirikiane na wafanyabiashara kuharakisha maendeleo ya wananchi mliokabidhiwa kuwaongoza. Acheni kudai hongo, kwani badala ya kuwasadia jamii, mtajikuta ninyi ndo mnakuwa vikwazo vya maendeleo,” alionya.
Alisema Serikali za Mitaa zinapaswa kuwa wawezeshaji na siyo wakwamishaji wa masuala ya maendeleo.
Ili kufanikisha hilo, aliwataka wakuu wa mikoa waanzishe eneo moja la biashara katika ngazi ya mkoa na halmashauri ili wawekezaji wanapofika katika mikoa yao, wasizungushwe na kukatishwa tamaa kwa sababu ya mlolongo wa taasisi zilizopo.
Alisema kila mmoja, hana budi kudumisha amani na utulivu wa nchi ili uwekezaji uweze kufanikiwa na kushamiri.
 “Hakuna uwekezaji endelevu na wenye tija katikati ya fujo na migogoro, na uwekezaji utashamiri pale tu penye amani na utulivu,” alisisitiza.
Mapema, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwezeshaji na Uwekezaji), Dk Mary Nagu alisema ili uwekezaji uweze kuwanufaisha wananchi ni lazima rasilimali za nchi zigeuzwe kuwa bidhaa.

No comments: