PINDA AAHIDI SERIKALI KUONDOA MATATIZO MIRADI YA NSSF



Serikali i imesema itajipanga  kuona namna ya kukabili  changamoto  zinazokwamisha miradi mikubwa, inayoendeshwa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF)  kwa lengo la kubadilisha sura ya Jiji la Dar es Salaam.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alisema hayo baada ya kutembelea miradi mitatu mikubwa inayoendeshwa na NSSF,  ikiwemo ujenzi wa daraja la Kigamboni.
Miradi mingine ni mradi wa nyumba za gharama nafuu inayojengwa Mtoni Kijichi na mradi wa nyumba zaidi ya 7,000 uitwao  ‘Dege Eco Village' huko Kigamboni.
Akizungumza wakati wa kukamilisha ziara yake  Kigamboni katika mradi wa nyumba  hizo, Pinda alisema Kigamboni inaendelea kwa kasi kubwa, kiasi kwamba miundombinu iliyopo haitoshi kuhimili idadi ya watu watakaohamia.
“Tunahitaji kujipanga kwa dhati kuhakikisha barabara na vivuko vinafanya kazi. Changamoto kubwa hapa ni barabara za viungo kutoka Mandela upande wa Kurasini na upande wa Kigamboni pia. Barabara hizi zote sita za darajani, zitatakiwa kufika Kigamboni, Mjimwema, Mbagala na kwingineko,” alisema.
Pinda alisema daraja litakapokamilika, watumiaji watatozwa  tozo la barabara ili kuweza kulihudumia. Alisema serikali inafikiria pia namna ya kuipanga Kigamboni ili iendane na maendeleo yanayokuja.
Kuhusu mradi huo wa Dege Eco Village wenye uwezo wa kuchukua nyumba za ghorofa zaidi ya 7,000 na za kawaida  300, Waziri mkuu alisema mradi huo utaleta msukumo mkubwa kwa maendeleo ya taifa.
Pinda alifurahishwa na kitendo cha NSSF, kuwapa kipaumbele wanachama wake kupata nyumba ambazo zimejengwa katika mradi wa mfuko huo uliopo Mtoni Kijichi.
Tayari nyumba 85 zilizojengwa katika awamu ya kwanza, zimeshachukuliwa na wanachama. Ujenzi wa nyumba hizo ulianza Novemba 2008 na kukamilika 2010.
Nyumba 215 zilizojengwa katika awamu ya pili,  zimeshachukuliwa na wanachama na wadau wengine. Kwa  mujibu wa Meneja Miradi, John Msemo, zilianza kujengwa mwaka 2011 na kumalizika mwaka jana, ikiwa ni awamu ya tatu.
Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Dk Ramadhani Dau alisema miradi yao ilikuwa inapata changamoto kubwa, hasa upande wa barabara.
“Tukimaliza ujenzi wa daraja tunategemea barabara zote jijini ziwe zimeisha ili kupunguza msongamano katika daraja. Itakuwa haina maana kumaliza daraja wakati maungio hayajakamilika,” alisema.
Aliongeza pia kuwa kumekuwa na changamoto mbalimbali katika kutekeleza wa miradi hiyo, ikiwemo ya kutopata ardhi kutoka kwa wananchi kwa muda unaofaa, serikali kuchelewa kutoa asilimia 40 ya sehemu yake katika mradi na pia masuala ya kitaalamu katika ujenzi wa daraja.

No comments: