PINDA AAGIZA JIJI LA MBEYA KUONGEZA MAPATO

Waziri Mkuu Mizengo Pinda ameutaka uongozi wa Jiji la Mbeya, kuongeza mapato yake ya ndani kwa kuweka mifumo ya kisasa ya ukusanyaji mapato.
Alitoa agizo hilo juzi wakati akizindua stendi ya kisasa ya mabasi katika eneo la Nanenane, nje kidogo ya Jiji la Mbeya.
“Nikuombe Meya Kapunga, wewe na watu wako ongezeni mapato ya ndani ya Jiji la Mbeya. Wekeni mifumo ya kisasa ya makusanyo inayotumia teknolojia ya habari na mawasiliano, acheni kutumia risiti za kuandika wa mikono,” alisema.
Akizungumzia mradi wa stendi mpya ya mabasi, Waziri Mkuu alisema ujenzi wa stendi hiyo ni miongoni mwa kazi zilizo kwenye mradi mkubwa, unaohusisha uboreshaji wa huduma na miundombinu kwenye miji na majiji saba hapa nchini.
Alisema mradi huo uliibuliwa na Serikali mwaka 2006 kwa kushirikiana na Benki ya Dunia. Miji na majiji mengine yanayotekeleza mradi kama huo ni Mwanza, Arusha, Tanga, Kigoma, Mtwara na Dodoma.
 “Utekelezaji wa miradi katika miji na majiji haya saba, umetuwezesha kupata ufadhili katika awamu ya pili ya mradi huu ambayo itajumuisha miji 17. Tusingekubaliwa kuingia awamu ya pili kama ninyi madiwani msingesimamia vizuri miradi hii,” alisema.
 Akisoma taarifa ya mradi huo, Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya, Mussa Zungiza alisema ujenzi wa stendi hiyo yenye ukubwa wa meta za mraba 30,000 utasaidia kupunguza msongamano wa magari kwenye barabara kuu ya Tanzam, ambako mabasi ya mikoani yalikuwa yakisimama na kupakia ama kushusha abiria.
 Alisema mradi huo wa stendi ya Nanenane, uliogharimu Sh bilioni 2.9 ni sehemu tu ya mradi mzima ambao thamani yake ni Sh bilioni 31.4, ambazo zimetumika kujenga barabara za kiwango cha lami zenye urefu wa kilometa 23.1, daraja moja na dampo la kisasa la kutupia taka (sanitary land fill) katika kata ya Nsalaga.
 Hata hivyo, mradi huo uko chini ya uangalizi wa mkandarasi hadi Desemba 4, 2014 utakapokabidhiwa rasmi kwa Halmashauri ya Jiji.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Pinda ameutaka uongozi wa Jiji la Mbeya kuhakikisha unatengeneza kwanza miundombinu ya maji na vyoo katika eneo jipya lililopo jirani na stendi mpya ya Nanenane ambalo limetengwa mahsusi kwa ajili ya wafanyabiashara ndogondogo maarufu kama ‘wamachinga’.

No comments: