NEC YAELEZEA MASHARTI YA DAFTARI LA WAPIGAKURA

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga kura linalotarajiwa kuanza hivi karibuni linamhusu kila raia mwenye sifa ya kupiga kura.
Ufafanuzi huo ulitolewa wakati kukiwa na mawazo tofauti ya nani hasa anatakiwa kushiriki katika zoezi hilo huku baadhi ya watu wakidhani kuwa jambo hili linawahusu ambao hawakuwahi kujiandikisha kupiga kura ama waliopoteza kadi na waliofikia umri wa kupiga kura.
Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu Damian Lubuva alisema juzi jijini Dar es Salaam kuwa katika kufanya maboresho hayo na kupata daftari linaloaminika zaidi, Tume inatarajia kutumia mfumo mpya wa utambuzi wa watu kwa alama za binadamu yaani “Biometric Voters Registration System”.
Alisema kwa kutumia mfumo huu, mhusika atachukuliwa alama za vidole vyote 10 vya mikono, picha na saini yake na ni tofauti na mfumo uliokuwa unatumika wa “Optical Mark Recognition” (OMR) uliohitaji kujaza fomu na alama ya kidole kimoja tu.
“Watu wote wenye sifa watatakiwa kujiandikisha upya katika mfumo huu mpya na kupatiwa kadi mpya,” alisema na kuongeza kuwa uboreshaji wa daftari hilo unatokana na matakwa ya kisheria na malalamiko ya wadau mbalimbali.
Alisema tangu uchaguzi mkuu mwaka 2010 pamekuwa na malalamiko kutoka kwa wadau kama vyama vya siasa, mashirika yasiyo ya kiserikali na wapiga kura kuhusu haja ya kuboresha daftari hilo. Sheria inataka liboreshwe mara mbili kati ya uchaguzi uliofanyika na ujao.
Akizungumzia matayarisho ya zoezi hilo, Mkurugenzi wa Uchaguzi, Julius Mallaba alisema yanaridhisha na kuendelea vizuri.
“Sehemu kubwa ya maandalizi yamekamilika,” alisema na kuongeza kuwa tayari ununuzi wa vifaa vya uandikishaji ikiwamo Biometric Voter Registration Kits umeshafanyika.
Alisema vituo katika ngazi ya vitongoji, vijiji na mitaa vimeongezeka kutoka vya awali 24,919 na kufikia vituo 40,015 nchi nzima.

No comments: