MWANAMKE AUAWA KIKATILI MKOANI TABORA



Mwanamke mkazi wa kijiji cha Tuombemungu Kata ya Ugunga wilaya ya  Kaliua mkoani Tabora, Mawazo Saidi, ameuawa kikatili.
Mume wa mwanamke huyo anatuhumiwa kufanya mauaji hayo, kwa madai ya kudaiwa fedha za tumbaku.
Mawazo aliuawa baada ya kutokea ugomvi kati yake na mumewe, unaodaiwa kusababishwa na fedha za mauzo ya tumbaku.
Mwenyekiti wa kijiji cha Tuombemungu, Abdulrahman  Anthony alisema tukio hilo ni la saa 6 usiku wa Agosti  15 mwaka huu.
Inadaiwa kuwa Ally  Jinasa,  ambaye ni mume wa mwanamke huyo, alirudi nyumbani akitokea katika kilabu cha pombe na kuanza kubishana na mkewe kuhusu fedha za tumbaku, ambazo mkewe alitaka kufahamu zilikokwenda.
Inadaiwa mwanamke huyo alijaribu kumsihi mumewe, kuachana na pombe kwani inarudisha nyuma maendeleo ya familia.
Pia, inadaiwa alimtaka aache kuuza tumbaku kwa walanguzi, badala yake aiuze kwenye chama cha  msingi ili fedha zitakazopatikana, zisomeshe mtoto wao shule.
Inadaiwa kuwa mume, Jinasa, alipinga ushauri huo na kisha kumkata mkewe huyo kwa panga kichwani na shingoni na kusababisha ubongo kusambaa. Alifariki dunia wakati akipelekwa hospitali kwa matibabu.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tabora, Suzan Kaganda (pichani) akizungumzia tukio alisema mtuhumiwa ametiwa mbaroni na atafikishwa mhakamani muda wowote upelelezi utakapomilika.

No comments: