MTOTO WA SHULE ZA KATA AIBUKA KIDEDEA SHINDANO LA INSHA SADC



Watoto wa Kitanzania kutoka shule za kawaida na zile za kata, wameendelea kuipa nchi heshima kimataifa, kwa kuongoza katika mashindano ya kitaaluma.
Jana mwanafunzi wa Kidato cha Nne katika Shule ya Sekondari Naboti iliyopo Makambako mkoani Njombe, Neema Mtwanga (16), aliibuka mshindi wa kwanza miongoni mwa washindani 39 katika Shindano la Utunzi wa Insha,lililoandaliwa na Jumuiya ya Maendeleo ya kusini mwa Afrika (SADC).
Huo ni ushindi wa pili kwa watoto wa Kitanzania kimataifa, baada ya Peter Kilave, ambaye alikuwa mwanafunzi wa kidato cha tatu wa Shule ya Sekondari ya Kata ya Tushikamane ya mjini Morogoro, kushinda tuzo ya Insha bora katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) mwaka jana.
Ushindi wa Neema ulitangazwa jana katika mji wa kitalii wa Victoria Falls nchini Zimbabwe, kunakofanyika mkutano wa 34 wa wakuu wa nchi za SADC. Neema alipongezwa na Rais Jakaya Kikwete, aliyepo nchini humo kuhudhuria mkutano huo.
Kutokana na ushindi huo, Neema alitunukiwa tuzo ya ushindi huo, hundi ya dola za Marekani 1,500 ambayo  ni sawa na Sh milioni  2.3 na amelipiwa gharama zote za kushiriki katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi za SADC. Pia, amepewa zawadi ya Ipad kwa ajili ya matumizi yake ya teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama).
Nafasi ya pili imeshikwa na Kudzai Ncube kutoka Shule ya Sekondari ya Mazowe nchini Zimbabwe. Nafasi ya tatu imeshikwa na Manxoba Msibi kutoka Shule ya Sekondari ya Etjendlovu katika Swaziland.
Insha 39 zilipokewa kutoka nchi 13 kati ya nchi 15 wanachama wa SADC, ikiwa ni insha tatu kwa kila nchi. Insha  hizo zilitoka Tanzania, Angola, Botswana, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Lesotho, Malawi, Mauritius, Msumbiji, Namibia, Afrika Kusini,  Swaziland,  Zamibia na Zimbabwe.
Majaji wa kupitia na kuamua washindi wa insha hizo walitoka Tanzania, Zambia na Zimbabwe na walikutana mjini Gaborone, Botswana, mwezi Julai mwaka huu kupitia insha zote na kutoa uamuzi wa washindi.
Akizungumza namwandishi, Mkuu wa Shule hiyo, Mwalimu Akulasi Kyando alisema amepokea kwa furaha ushindi huo na hasa baada ya Neema kuzingatia maelekezo waliyompa.
“Tumefurahi, tena ameitangaza shule, tulimpa moyo kwa kuwa tunamfahamu ni mwandishi mzuri mpaka hata nyie mmemfahamu,” alisema.
Mwalimu Kyando alisema Neema ni mwanafunzi mwenye tabia nzuri na kwa kudhihirisha hilo, yeye ndiye Dada Mkuu wa shule hiyo.
Kwa mujibu wa Mwalimu Mkuu huyo, hata katika taaluma, Neema amekuwa na matokeo mazuri na hata mtihani wa mock wa kidato cha nne uliofanyika hivi karibuni, alipata daraja la kwanza.
Mwandishi alitaka kujua mazingira anayotokea Neema, ambapo mwalimu wake alisema anatoka kijijini katika Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa na kuongeza: “Ni kijijini na ni mtoto wa mkulima tu.”
Ofisa Elimu wa Mkoa wa Njombe, Said Nyachiro, alisema ofisi yake ilipata taarifa ya kuwepo kwa shindano hilo na kupeleka kwa wakuu wote wa shule zilizopo katika mkoa huo.
Alisema mbali na kusambaza taarifa hizo katika mabango, wamekuwa wakiwasihi walimu kusaidia wanafunzi wenye uwezo, kushiriki katika mashindano hayo.
Alisema amefurahi baada ya kupata habari za mwanafunzi kutoka Njombe, kuongoza nchi 13 za SADC.
Wanafunzi waliopenda kushiriki katika shindano hilo, walitakiwa “Kutoa mapendekezo ya nini kifanyike katika sekta ya elimu, ili kupunguza athari za mabadiliko ya tabia nchi kwa vijana”.
Katika utangulizi wa insha hiyo, mwanafunzi alitakiwa kuhakikisha anamvutia msomaji kwa kutambulisha mada na kuanza kujadili. Msisitizo katika utangulizi, ulikuwa kumtambulisha msomaji mada na kumuingiza katika mjadala.
Alitakiwa kueleza namna anavyofahamu mabadiliko ya tabia nchi na ongezeko la joto duniani, kwa kutoa utambulisho wa moja kwa moja katika aya moja au mbili tu.
Katika kujadili, mwanafunzi alitakiwa kuanza kujadili mada kwa kufuata utaratibu uliowekwa bayana, na aliruhusiwa kuweka vichwa vya habari kwa ufupi kutoka hoja moja kwenda nyingine.
Katika utaratibu huo wa usahishaji, wanafunzi walitakiwa kujadili kwa kuzingatia mgawanyo wa sehemu tano muhimu za insha hiyo na waliruhusiwa kuweka vichwa vya habari kwa ufupi, kutambulisha sehemu husika.
Sehemu ya kwanza ya insha hiyo, ilipaswa kuelezea sababu za mabadiliko ya tabia nchi, ilikuwa na alama kumi kati ya alama mia moja za insha nzima. 
Sehemu ya athari za ongezeko la joto duniani na mabadiliko ya tabia nchi katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi, ilipewa alama 20 kati ya alama mia moja za insha hiyo.
Aidha, sehemu ya kwanza kwa alama nyingi ni mafanikio na wapi paliposhindikana katika utekelezaji wa Mkataba wa Kimataifa wa Kyoto, uliotaka nchi zenye viwanda kupunguza utoaji wa hewa ukaa ambao ulianza kutekelezwa mwaka 2005. Sehemu hiyo ilikuwa na alama 25.
Pia mwanafunzi alitakiwa kueleza changamoto katika kushughulikia athari za mabadiliko ya tabia nchi na sehemu hiyo ilikuwa na alama 20.
Sehemu ya mwisho kabla ya hitimisho, ambayo nayo imepewa alama nyingi yaani 25 kati ya 100, mwanafunzi alitakiwa kutoa ushauri nini kifanywe na sekta ya elimu katika nchi za SADC ili kupunguza athari za mabadiliko ya tabia nchi.
Wanafunzi wote waliopenda kushiriki, walitakiwa kuwa makini na alama zilizopangwa katika kila sehemu, hivyo wasahishaji walitarajia aya ziwe nyingi katika sehemu ambazo zimewekewa alama nyingi.
Katika hitimisho la insha hiyo, mwanafunzi alitakiwa kueleza kwa ufupi hoja muhimu alizozitetea katika mjadala na alipaswa kuweka msisitizo kuhusu nini angependa kifanywe na nchi wanachama wa SADC katika kupunguza athari za mabadiliko ya tabia nchi katika Ukanda huo.
Wanafunzi pia waliwekewa onyo kwa msisitizo dhidi ya atakayeiga insha kuwa ni kola la kitaaluma. Lakini pia waliruhusiwa kuomba ushauri kutoka kwa walimu na kufanya marejeo kutoka katika vyanzo vinavyotambulika.

No comments: