MTOTO AFA MAJI KWENYE NDOO

Mtoto wa umri wa mwaka mmoja amekufa baada ya kutumbukia kwenye ndoo ya maji nyumbani kwao, wakati akicheza.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Kihenya wa Kihenya, tukio hilo ni la juzi saa 4:30 asubuhi katika eneo la Buza.
Alisema mtoto huyo, Najma Omary alikuwa akicheza nje ya nyumba yao  kulikokuwa na ndoo ya maji na alitumbukia kwa kutanguliza kichwa na kunywa maji mengi yaliyosababisha mauti yake.
Kamanda Kihenya alisema maiti ya mtoto huyo imehifadhiwa hospitali ya Temeke na hakuna mtu anayeshikiliwa na Polisi na kwamba uchunguzi zaidi wa tukio hilo unaendelea kufanywa.
Katika tukio la pili, watu 14 wamekamatwa na polisi katika mikoa miwili tofauti ya kipolisi kwa tuhuma za kukutwa na pombe haramu ya gongo pamoja na misokoto ya bangi.
Kamanda Kihenya alisema  Polisi waliendesha msako juzi asubuhi maeneo ya Kingungi kwa Nyoka, huko Kiburugwa na kuwakamata watu tisa wakiwa na bangi puri moja na kete 92. Watuhumiwa hao wanashikiliwa na watafikishwa mahakamani.
Katika tukio jingine, Kamanda wa Polisi mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura alisema Polisi walifanya msako  juzi saa 4:30 asubuhi maeneo ya Msasani na kukamata watuhumiwa watano wakiwa na pombe haramu ya gongo.
Kamanda Camillius alisema watuhumiwa hao walikutwa na lita 60 za pombe hiyo haramu  na kwamba watafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.

No comments: