MSAIDIZI ALIYECHOMWA MWILINI AELEZEA MADHILA YA MWAJIRI WAKEMsichana Yusta Kashinde (20) aliyejeruhiwa kwa kuchomwa na pasi na kung'atwa sehemu za mwili na mwajiri wake Amina Maige (42), ametoa ushahidi wake mahakamani na kueleza kuwa mshitakiwa alimpiga na alipochoka, alimng’ata.
Alitoa ushahidi wake jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni, mbele ya Hakimu Yohana Yongolo kwa muongozo wa wakili wa serikali Tumaini Mfikwa. Alidai alipomaliza elimu ya msingi katika Shule ya Kampala, mkoani Tabora, aliletwa Dar es Salaam kwa makubaliano ya mama yake.
Alidai walikubaliana na mwajiri huyo kuwa anakuja jijini hapa kumfanyia kazi za ndani na alipofika mwaka 2010 alimkuta akiwa na kaka yake, mumewe na watoto wake. Alidai baadae mumewe aliondoka akiaga anakwenda shule kusoma na watoto pia waliondoka kwa muda mrefu na tangu wakati huo mama huyo alianza kumpiga mara kwa mara.
Kashinde alidai mshitakiwa alikuwa akimpiga sehemu mbalimbali za mwili kwa mkono na alipochoka alimng’ata.
Hakimu Yongolo aliamuru kesi ihamie katika chumba maalumu kupata ushahidi wa sehemu za mwili zilizong’atwa na mahakama ilihamia kwa muda katika chumba maalumu. Kesi hiyo baadae iliahirishwa hadi leo.

No comments: