MKATABA KUJENGA CHUO KIKUU CHA SAYANSI NA HISABATI WASAINIWA

Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imesaini Mkataba wa Ushirikiano (MOU) baina yake na Taasisi ya Masuala ya Sayansi na Hisabati Afrika (AIMS), kwa ajili ya kuanzisha Chuo Kikuu cha masuala ya sayansi na hisabati, kitakachojengwa wilayani Bagamoyo mkoani Pwani.
Akizungumza na waandishi wa habari katika hafla ya utiaji saini Mkataba huo, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Profesa Sifuni Mchome, alisema Mkataba huo utawezesha Serikali ya Tanzania na taasisi hiyo kwa pamoja kujenga na kusimamia chuo hicho nchini.
Alisema hadi sasa tayari maandalizi ya uanzishwaji wake yamekamilika na Wakala wa Nyumba nchini (TIB) imetoa eneo la Boma mjini Bagamoyo kwa ajili ya kuanzisha chuo hicho kitakachosimamia masuala yote ya mafunzo ya sayansi na hisabati.
“Kwa sasa bado mazungumzo ya namna ya kuanzisha chuo hiki yanaendelea, ila imekubaliwa kuwa kwa kuanzia, tayari wanafunzi 40 wameshadahiliwa na watajiunga na chuo hicho katika Chuo cha Nelson Mandela jijini Arusha, Septemba mwaka huu, hadi pale chuo cha Bagamoyo kitakapokamilika,” alisema Profesa Mchome.
Alisema chuo hicho kitakachotoa Shahada ya Sayansi na Hisabati, kitasaidia kuondoa tatizo la wataalamu wa masuala ya sayansi nchini, walimu na wataalamu wa sekta nyingine nyeti kama vile madaktari, walimu na wahandisi ambao wote wanategemea elimu ya sayansi na hisabati ili kutimiza wajibu wao.
Alisema matarajio ya Tanzania katika sekta ya elimu kupitia Mpango wake wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) hadi mwaka 2025, ni kuwa nchi inayozalisha wataalamu wenye ubora katika nyanja zote ikiwemo maeneo ya sayansi na teknolojia na hivyo kuchangia kukuza uchumi wa nchi hiyo bila kutegemea wataalamu wa nje ya nchi.
Naye Mtendaji Mkuu wa taasisi hiyo ya AIMS, Thierry Zomahoun, alisema ili Tanzania iwe imekamilika kiuchumi na kitaalamu ni lazima iwekeze nguvu zake katika kuhamasisha elimu ya sayansi na hisabati.

No comments: