MKAPA ACHOMOZA UCHUMI WA VIWANDA NCHINI



Uongozi wa Awamu ya Nne chini ya Rais Benjamin Mkapa, umetajwa kwamba ndio uliojenga msingi wa uanzishwaji wa viwanda vya ndani nchini kupitia mfumo wa kodi.
Mbunge wa Singida Mjini, ambaye pia ni mmoja wa wafanyabiashara wenye viwanda, Mohamed Dewji, amesema hayo mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam, alipokuwa akiingia mkataba wa ushirikiano na kampuni ya RMB.
“Katikati ya miaka ya 1990 Rais Benjamini Mkapa aliingia madarakani akaanzisha mfumo wa kodi ambao ulilazimisha uchumi kujenga msingi wa viwanda vya ndani,” alisema Dewji.
Kwa mujibu wa Dewji, kabla ya hapo wafanyabiashara wa Tanzania, walikuwa wakipata faida kwa kuagiza kutoka nje ya nchi karibu kila kitu, kutoka karatasi za chooni mpaka dawa za meno.
Alisema Mkapa alipoingia madarakani, alianzisha mfumo wa kodi ambao ulimlazimisha mfanyabiashara kuacha kununua bidhaa zilizotengenezwa viwandani nchi za nje na kununua malighafi ili atengeneze bidhaa hapa nchini.
Mfumo huo wa kodi kwa maelezo ya Dewji, ulimtoza mfanyabiashara anayeagiza kutoka nje bidhaa zilizo tayari kuuzwa katika soko la ndani, asilimia 25 ya thamani ya bidhaa hiyo.
Kwa mfanyabiashara aliyeagiza bidhaa ambayo bado ina ughafi kidogo (semi finished), ambayo itatakiwa kuingizwa katika viwanda vya ndani kuondolewa ughafi ndio iuzwe katika soko la ndani, mfumo huo ulimpa unafuu kwa kumtoza kodi ya asilimia 10 ya bidhaa hiyo.
Dewji alisema mfanyabiashara aliyeagiza malighafi kabisa, ambayo ilipaswa kuingia katika viwanda vya ndani ili kutengeneza bidhaa ya kuuza katika soko la ndani, alipata nafuu kubwa kwa kuwa hakutozwa kodi ya aina yoyote.
“Nilitambua fursa kubwa iliyokuwa hapo, baba yangu alikuwa akiagiza mafuta ya kula, nikafikiria kwa nini nisianzishe kiwanda cha mafuta ya kula, lakini akaona ni hatua ya hatari kibiashara.
“Nilimkopa dola za Marekani milioni moja na kununua kiwanda cha sabuni kinachozalisha tani 24 za sabuni kwa siku, leo kinazalisha tani 500 kwa siku. Niliendelea nikanunua kiwanda cha kwanza cha mafuta ya kula chenye uwezo wa kuzalisha tani 60 za mafuta ya kula kwa siku,” alisema Dewji.
Kwa mujibu wa Dewji, kwa sasa kiwanda hicho cha mafuta ya kula kinazalisha tani 2,200 kwa siku na ndio kiwanda kikubwa cha mafuta ya kula Afrika huku kampuni ya Mohammed Enterprises Ltd (MeTL), ikitarajia kuongeza pato lake la mwaka hadi dola bilioni tano na kutoa ajira rasmi laki moja ifikapo 2018.
Dewji ambaye kampuni yake inafanya biashara nyingi katika Ukanda wa Afrika ya Mashariki, Kati, Kusini mpaka nchi za Mashariki ya Kati, alisema pia aliingia katika kilimo cha katani, ambacho zao lake sasa lina soko jipya kimataifa.
Alisema zao hilo lilizoeleka kutengenezea kamba na kuwa malighafi katika viwanda vya meli na mashuwa,  leo linatumika kutengeneza mabodi ya magari aina ya Mercedes Benz na ndege katika Bara la Ulaya na katika nchi za Mashariki ya Kati, linatumika kutengeneza nyumba zinazozuia joto kuingia ndani.

No comments: