MJUMBE BUNGE LA KATIBA APIGA KURA AKIWA KITANDANI HOSPITALINI

Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kutoka kundi 201, Thomas Mgoli (pichani kushoto), ambaye alikuwa amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, amelazimika kupiga kura hospitalini, kushiriki kufanya uamuzi wa ibara alizoshiriki kujadili katika Kamati yake.
Akiwa hospitalini hapo, watendaji wa Bunge Maalumu la Katiba walimfuata na kumpa fursa ya kupiga kura kwa utaratibu wa kusema ‘Ndiyo’ au ‘Hapana’, kuhusu ibara 39 iliyopo katika sura ya 4 ya Rasimu ya Katiba mpya, inayozungumzia haki za binadamu, wajibu wa raia na mamlaka za nchi.
Ibara hiyo inataka wananchi wenye ulemavu kuruhusiwa kuingia popote na vifaa vinavyowasaidia,ambayo mjumbe huyo amepiga kura ya ‘Hapana’, akidai kuwa kifungu hicho kinatibua
usalama, kwani mlemavu akiruhusiwa kuingia mathalani na magongo, anaweza kuporwa na magongo hayo kutumika kufanya  shambulizi.
Alipoulizwa kama afya yake inastahili kupiga kura, alisema alishaandaliwa kisaikolojia na madaktari na kwamba maumivu yaliyopo sasa ya kichwa na shingo, hayawezi kumzuia kufanya uamuzi.
Mgoli alipigwa na kulazwa Hospitali ya Mkoa wa Dodoma na wanaodhaniwa kuwa wafuasi wa kundi la Umoja wa  Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Kutokana na hali hiyo, Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta amewaonya wajumbe wa bunge hilo, kuacha kuhamishia mijadala baa, kwani ni hatari kwa maisha yao.

No comments: