MAFUNDI GEREJI WA TEGETA WAPELEKWA MABWEPANDE

Serikali imewataka wananchi wanaojulikana kama Umoja wa Mafundi Gereji, waliopo eneo la Tegeta Wazo Hill jijini Dar es Salaam  kuondoka eneo hilo kabla ya Agosti 17 mwaka huu na kuhamia eneo walilotaarifiwa, ili kutekeleza amri ya Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick jana na kuwataka mafundi hao kuhamia eneo la Nyakasangwe lililopo Kata ya Mabwepande.
Akitoa agizo hilo, mara baada ya kutembelea eneo hilo la Nyakasangwe akiongozana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa, aliwataka wafundi hao kutii agizo hilo ili na kuepuka malumbano.
Aidha, ametoa siku tatu kwa mafundi hao, kuanzia kesho hadi Agosti 13, mwaka huu wawe wameshaondoka eneo hilo na wafike katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri Wilaya ya Kinondoni, ili kujiandikisha na kuendelea na utaratibu ulioandaliwa.
Umoja huu umekuwa ukifungua kesi mahakamani mara kwa mara kudai uhalali wa eneo hilo lakini mnamo Juali 18, mwaka huu, Mahakama Kuu kitengo cha Ardhi ilitoa amri ya wananchi hao kuondoka eneo hilo kabla ya Agosti 17, mwaka huu.
Alisema kwa busara, uongozi wa Mkoa ulimwomba mwekezaji Nyanza Road Works, kuwasaidia mafundi hao kupata eneo lingine ili wahamie, ndipo alipotoa eneo hilo lenye ukubwa wa hekari 37, ili ligawanywe kwao kulingana na utaratibu utakaowekwa.
Kadhalika mkuu huyo alitoa onyo kwa mtu yoyote atakayekaidi agizo hilo kuwa atachukuliwa hatua kali za kisheria ikiwa ni pamoja na kufikishwa Mahakamani.

No comments: