KITUO CHA SHERIA CHAWAVAA WAJUMBE BUNGE LA KATIBA


Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimeshauri wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kuheshimu uhuru wa kutoa maoni na kupokea habari kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kimesema ni vyema wadau wote wakaepuka kutoa kauli zitakazokuwa chanzo cha kuzorotesha umoja na amani kwa Taifa.
Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Dk Hellen Kijo-Bisimba alisema hayo Dar es Salaam wakati akizungumzia mwenendo wa mchakato wa utungwaji wa Katiba mpya na kuongeza kuwa wananchi wapewe uhuru wa kujadili hatma ya taifa lao kupitia mchakato  huo wa  Katiba mpya.
“Hii ni pamoja na wajumbe wa Bunge la Katiba kuheshimu mawazo ya wananchi yaliyomo ndani ya Rasimu ya pili ya Katiba haswa ikifahamika kuwa kila mtu anao uhuru wa kuwa na maoni na kueleza fikra zake, kuwa na haki ya kutafuta, kupokea na kutoa habari bila kujali mipaka ya nchi,” alisema Dk Bisimba.
Kwa mujibu wa Katiba,  kila mtu ana uhuru wa kufanya mawasiliano na haki ya kutoingiliwa katika mawasiliano hayo na pia ana haki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbalimbali muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi na pia kuhusu masuala muhimu kwa jamii.
Kwa upande wake, mpigania haki za Watanzania, Ananilea Nkya aliwashauri viongozi waliopo katika Bunge Maalumu la Katiba kutumia busara na ujasiri walio nao katika kuhakikisha wanasimamia haki na kupata suluhu na kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

No comments: