KIKWETE APUUZA MADAI YA KUMWOKOA RIDHIWANI CHINA

Rais Jakaya Kikwete amesema madai kuwa yeye alishiriki kumwokoa mtoto wake, ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Chalinze, Ridhiwani Kikwete, baada ya kukamatwa na dawa za kulevya nje ya nchi, ni mkusanyiko wa upuuzi mtupu.
Aidha alisema kuwa urais ni taasisi kubwa nchini na yeye akiwa Rais hawezi kujiingiza katika ubishani na watu wa mtaani, kama ambavyo wanataka baadhi ya watu wanaomsukuma ili ashiriki katika maneno hayo ya mitaani.
“Ni mkusanyiko wa upuuzi. Sina muda wala siwezi kupoteza nguvu yangu kujadili upuuzi na ujinga wa namna hiyo,” alisema Rais Kikwete usiku wa mwishoni mwa wiki, wakati alipozungumza na Watanzania wanaoishi Marekani, mjini Washington D.C.
Rais Kikwete ambaye yuko katika ziara ya kikazi ya siku tisa   Marekani, alitoa majibu hayo baada ya kuulizwa kuhusu madai yaliyotolewa Julai Mosi, mwaka juzi  na Katibu Mkuu wa  Chadema, Willibrod Slaa, ambayo yamempeleka mahakamani.
“Hatuwezi sisi kujiingiza katika shughuli ya kupoteza muda kwa kushiriki upuuzi na ujinga. Haya ni maneno ya kipuuzi yanayosemwa na watu ambao kazi yao usiku na mchana ni kuota jinsi ya kuyumbisha ajenda yetu ambayo imefanikiwa sana katika kubadilisha hali ya maisha ya Watanzania.
“Urais ni taasisi kubwa sana. Rais wa nchi yetu hawezi kujiingiza katika ubishani na watu wa mitaani. Kwanza huyo Ridhiwani amemfikisha Slaa kortini na mpaka leo hata kesi yenyewe haijatajwa,” alisema.
Kuhusu madai kwamba Rais Kikwete alitia saini mikataba 12 na uongozi wa Jamhuri ya Watu wa China, kama sehemu ya masharti ya kuachiwa kwa Ridhiwani, Rais Kikwete alisema:
“Naipenda nchi yangu kiasi cha kwamba siwezi kufikiria hata kuiweka rehani. Haya ni maneno ya kipuuzi tu yenye kutafuta kututoa kwenye ajenda zetu nzuri. Hatuna muda nayo, sisi tunaelekeza nguvu zetu kwenye mambo ya maana ya kuleta mabadiliko katika ustawi wa Watanzania,” alisema.

No comments: