KANUNI MPYA ZA KUKOKOTOA MAFAO ZATANGAZWA


Serikali imetangaza kanuni mpya, mbazo zinatoa viwango sawa vya vikokotoa kwa mifuko yote ya hifadhi ya jamii, ambapo sasa watalipwa asilimia 72.5 kutoka asilimia 60-67 kwa baadhi ya mifuko iliyokuwa ikilipwa awali.
Pia, kiwango cha chini cha pensheni, kimeongezwa kwa mifuko ambayo haikuwa na kiwango cha chini.
Kwa sasa kiwango cha chini, kitakuwa asilimia 40 ya kima cha mshahara wa sekta husika.
Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudentia Kabaka, akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari mjini hapa jana, alisema Sera ya Taifa ya Hifadhi ya Jamii ya mwaka 2003, imeainisha changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya hifadhi ya jamii, ikiwemo kupishana kwa vikokotoa vya mafao.
Alisema utofauti wa vikokotoa hivyo, umeleta malalamiko mengi kutoka kwa wanachama, kwa kuwa vimesababisha kuwepo kwa tofauti kubwa ya viwango vya pensheni, vinavyotolewa na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.
Alieleza kuwa kutokana na hali hiyo, Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) kwa kushirikiana na Wizara ya Kazi na Ajira na wafanyakazi na waajiri, imechukua hatua mbalimbali kutatua changamoto ili kuboresha changamoto hizo.
Alisema hatua hiyo ni pamoja na kurekebisha sheria zote za Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ili ziendane na matakwa ya Sheria ya Hifadhi ya Jamii Namba 8 ya mwaka 2008 na SSRA imeshatoa miongozo mbalimbali, inayolenga kuboresha sekta ya hifadhi ya jamii kwa manufaa ya wanachama.
Alisema kanuni hizo, zinatoa fomula moja kwa mifuko yote ya lazima ya pensheni ;na zimelenga maeneo makuu saba, ambayo ni kurekebisha vikokotoa limbikizi (accrual rates) vya mifuko yote.
“Hii itawezesha viwango vya vikokotoa hivyo kuongeza mafao ya wanachama ambao wamekuwa wakilalamika kwa muda mrefu.
“Wanachama wa NSSF, PPF na GEPF ambao wangepata asilimia 60-67 sasa watalipwa asilimia 72.5, hii pia itawafaidisha wanachama wa PSPF na LAPF mara watakapostaafu,” alisema.
Pia, eneo lingine ni kuthaminisha mafao ili kuendana na thamani ya kifedha na hiyo inatokana na kifungu kinachoelekeza hatua za uthaminishaji wa mafao kufanyika ili kuwafanya wastaafu, wanaopokea mafao kuendelea kuishi maisha yenye staha.
“Kuanzia sasa pensheni za wastaafu, zitathaminishwa kila baada ya tathmini ya kitaalamu kufanyika. Kiwango cha chini cha pensheni kimeongezwa hasa kwa mifuko ambayo haikuwa na kiwango cha chini ambayo ni PSPF, GEPF na LAPF. Hapa mstaafu anayepata pensheni ambayo ni ya chini ya asilimia 40 ya mshahara uliokokotolewa, atalipwa asilimia 40 ya kima cha  mshahara wa sekta husika,” alisema Waziri Kabaka.
Pia, alieleza kuwa eneo lingine ni kutumia wastani wa mshahara wa miaka mitatu, badala ya miaka mitano na hivyo kumwezesha mwanachama kulipwa vizuri zaidi.
“Hatua hii itasaidia kuondoa malalamiko kwa wanachama kwani wastani wa miaka mitano, ambao ulikuwa unatumiwa na baadhi ya mifuko unapungua mafao ya wanachama,” alisema.
Alieleza kuwa kanuni hizo, zinamruhusu mwanachama kuchagua kupokea asilimia 100 ya pensheni au kupokea mkupuo na baadaye kupata asilimia 75 ya pensheni.
“Hata hivyo kanuni izi hazitawagusa wanachama wa sasa wa Mifuko ya Pensheni ya PSPF na LAPF, kwa upande wa mifuko hiyo miwili ya PSPF na LAPF kanuni hizi zitawahusu wanachama wapya tu,” alisema na kuongeza kuwa kanuni hizo zilianza kutumika Julai Mosi mwaka huu.

No comments: