HAKIMU AHUKUMIWA FAINI MILIONI 1.5/- KWA RUSHWA YA MILIONI 2/-

Aliyekuwa Hakimu Mkazi Mahakama Wilaya ya Urambo, Oscar Bulugu, amekutwa na hatia ya kuomba na kupokea rushwa ya Sh milioni 2.
Mtu huyo amehukumiwa kwenda jela miaka mitatu, au kulipa faini ya Sh milioni 1.5.
Adhabu hiyo ilitolewa mwishoni mwa wiki na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mkoa wa Shinyanga, Massele  Chaba.
Alitoa hukumu hiyo katika Mahakama ya Mkoa Tabora, baada ya kuridhika na ushahidi wa upande wa mashitaka.
Katika hukumu hiyo iliyosomwa kwa saa mbili, Hakimu Chaba alisema analazimishwa na matakwa ya sheria, kutoa adhabu hiyo kwa mshitakiwa aliyetiwa hatiani , na endapo mshitakiwa hataridhika na uamuzi huo, anaweza kukata rufaa.
Bulugu alifikishwa mahakamani hapo mwaka jana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), akikabiliwa na mashitaka matatu;  moja la kuomba na mengine mawili ya kupokea rushwa.
Upande wa mashitaka ukiongozwa na Wakili Mabula Mapalala, ulidai kuwa mshitakiwa alitenda makosa hayo kati ya Machi 15 hadi 22 mwaka jana, wakati akiwa akiwa   Hakimu Mkazi wa Wilaya ya Urambo.
Ilidaiwa kuwa  Machi 15 mwaka jana, mshitakiwa alimshawishi Lucas Changala ampe Sh milioni tano ili ampe dhamana ndugu yake, aliyekuwa anakabiliwa na kesi ya wizi wa fedha za benki ya NMB.
Wakili Mapalala alidai katika shitaka la pili kuwa Machi  18 mwaka jana, mshitakiwa alipokea Sh milioni moja kutoka kwa Changala kama malipo ya awali  ili ampe dhamana Phillipo Raymond ,aliyekuwa mtumishi wa benki ya NMB, anayetuhumiwa kuiba zaidi ya Sh milioni mia moja.
Katika shitaka la tatu, Mwanasheria huyo wa Takukuru alidai kuwa Machi 21 mwaka huu, mshitakiwa huyo alipokea tena Sh milioni moja, ikiwa ni muendelezo wa malipo aliyoomba ili atoe dhamana kwa mtumishi huyo wa NMB.
Baada ya Mahakama kumtia hatiani mshitakiwa, upande wa mashitaka uliomba Mahakama itoe adhabu kali ili iwe fundisho, kwani wananchi wamekuwa wakilalamikia vitendo vya rushwa, hasa vinavyofanywa na watumishi wa umma.
Kwa upande wake, akijitetea, Bulugu aliomba asipewe adhabu kubwa, kwa vile ni mkosaji wa mara ya kwanza,  hana wazazi na ana familia ya watu zaidi ya kumi wanaomtegemea yeye, wakiwemo watoto wake baada ya kufiwa na mkewe.
Baada ya utetezi huo, Hakimu Chaba aliyesikiliza shauri hilo, alimhukumu alipe faini ya Sh 500,000 kwa kila kosa, ama kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela kwa kila kosa na adhabu hiyo ya kifungo itakwenda pamoja. Mshitakiwa alilipa faini hiyo na kuachiwa huru.

No comments: