FEDHA ZA MAPATO YA GESI KUANZA KUINGIA MWAKA 2020


Mapato yatokanayo na uwekezaji katika miradi ya gesi asilia, baada ya wawekezaji kutoa gharama zao za utafiti na uwekezaji, yataanza kupokewa nchini 2020.
Rais Jakaya Kikwete alisema hayo juzi alipozungumza kwenye Kituo cha Kimataifa cha Maendeleo mjini Washington DC, Marekani, ambako alizungumzia  hali ya baadaye ya Tanzania baada ya ugunduzi wa gesi. 
Alisema anataka na anatamani kuwa Rais wa mwisho wa Tanzania, kuongoza nchi ambayo ni masikini, hivyo atatumia muda wake uliobakia katika uongozi, kuelekeza nchi kwenye mwelekeo huo.
Aidha, Rais Kikwete alisema kuwa jambo la msingi la kama Watanzania watanufaika na ugunduzi wa gesi asili, ama watabakia katika hali yao ya sasa ya umasikini, ni la aina ya uongozi ambao nchi itaupata, uongozi wenye uwezo wa kufanya maamuzi sahihi kwa kadri nchi inavyozidi kusonga mbele.
Rais Kikwete yuko nchini Marekani kwa ziara rasmi ya siku tisa, ambako miongoni mwa mambo mengine, anahudhuria Mkutano wa Kwanza wa Viongozi wa Marekani na Afrika, ulioitishwa na Rais Barack Obama wa Marekani, ulioanza jana.
Rais Kikwete ameuambia mkutano kwenye kituo hicho, kuwa anataka kufanya kila linalowezekana katika kipindi chake kilichobakia cha uongozi, kuhakikisha anaanzisha na kuanza kujenga taasisi na kuweka kanuni sahihi za kusimamia rasilimali ya gesi asilia.
“Nitafanya kila linalowezekana kuhakikisha kuwa Watanzania na nchi yao, wananufaika kutokana na mapato ya rasilimali kutokana na gesi asilia. Nataka na natamani kuwa Rais wa mwisho wa Tanzania kuongoza nchi masikini.
“Rasilimali ya gesi inatoa nafasi na fursa kubwa kwa nchi yetu kuondokana na umasikini. Mimi nimeongoza nchi masikini, lakini nataka mrithi wangu kuongoza nchi yenye ustawi na utajiri,” alisema Rais Kikwete na kuongeza:
“Hivyo, dhamira na shughuli yangu kubwa kati ya sasa na mwisho wa kipindi changu cha uongozi ni kuiongoza nchi yetu kuelekea kwenye njia hiyo ambako gesi italeta ustawi na utajiri na maisha bora zaidi kwa wananchi wetu.”
Hata hivyo, Rais  Kikwete alisema kuwa ili Watanzania wanufaike na mapato ya gesi ni muhimu kuwepo na uongozi imara, ambao utakuwa tayari kuchukua maamuzi sahihi kwa kadri nchi inavyosonga mbele.
Tanzania ilianza kutafuta gesi na mafuta tangu miaka ya 1950. Ugunduzi wa kwanza ulikuwa 1974  katika Kisiwa cha Songo Songo Mkoa wa Lindi na Mnazi Bay Mkoa wa Mtwara mwaka 1982.
Hata hivyo ni mwaka 2010 ambapo ugunduzi mkubwa wa gesi, ulifanyika kwenye eneo la bahari, ugunduzi ambao mpaka sasa umefikia futi za ujazo trilioni 50.5.

No comments: