DIWANI 'SHEHE BWANGA' AFARIKI BAADA YA KUUGUA GHAFLA KIKAONI

Diwani wa Kata ya Mzingani (CCM), Fadhili Bwanga (60) maarufu kwa jina la ‘Shehe Bwanga’ amekufa akipatiwa matibabu ya awali katika Hospitali ya Mkoa wa Tanga ya Bombo (pichani) baada ya kuugua ghafla akiongoza kikao.
Bwanga alikutwa na mauti jana alasiri, baada ya kutolewa kikaoni ambako alikuwa akikaimu nafasi ya Mstahiki Meya. Kikao hicho kilijumuisha wajumbe wa Kamati ya  Mipango Miji ya Madiwani wa Manispaa ya Ilala Jijini Dar es Salaam iliyo kwenye ziara ya kikazi kutembelea eneo la mradi wa Pongwe City unaosimamiwa na Halmashauri ya Jiji la Tanga.
Baadhi ya watu waliokuwa katika kikao hicho walidai Bwanga alijisikia vibaya ghafla saa tisa kasoro alasiri akiwa kwenye  kikao na wageni hao ndani ya ukumbi wa Halmashauri ya Jiji  la Tanga na ndipo alipoomba kurudishwa nyumbani kwake eneo la Sahare na baadaye hali ilibadilika na kukimbizwa Hospitali ya Bombo.
Akizungumzia kifo cha diwani huyo, aliyekuwa pia Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Madiwani wa Jiji la Tanga, Mwenyekiti wa Kamati ya Mipango Miji ya Madiwani hao na diwani wa Mzizima, Dany Magaza alisema alimkabidhi Bwanga ugeni huo kutokana na yeye kuhitajika katika Kamati ya Siasa ya Wilaya.
“Mimi ndiye niliyekuwa mwenyeji wa ugeni huu lakini kwa sababu nilikuwa nahitajika
kwingine nikamwomba Shehe Bwanga aambatane nao kwa makubaliano kwamba baada ya ziara tutakutana ofisini kwa majumuisho ndipo ghafla napata simu kuwa amefariki kwa kweli nimeshtuka sana,” alisema Magaza.
Naye Naibu Meya wa Halmshauri ya Jiji hilo, Muzamil Shemdoe alisema kuwa Baraza la Madiwani limepoteza mtu makini kutokana na hekima zake na busara zilizochangia kuwakusanya pamoja madiwani bila kujali itakadi za vyama.
Kwa mara ya kwanza, Shehe Bwanga aliingia katika kinyang’anyiro cha
uchaguzi mwaka  2010 na kushinda Udiwani katika kata ya Mzingani aliyoiongoza mpaka  mauti ilipomkuta.

No comments: