DAKTARI ATIWA MBARONI KWA MADAI YA KUUA MGONJWA

Polisi mkoani Singida inamshikilia mtu anayedaiwa kuwa daktari ‘feki’ kwa tuhuma ya kusababisha kifo cha mgonjwa, mkazi wa kijiji cha Iyumbu, Wilaya ya Ikungi mkoani hapa.
Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Dk Philip Kitundu alimtaja Prosper Samson anayetuhumiwa kusababisha kifo cha Jubulu Mahende ambaye alikuwa mgonjwa.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Singida, Geofrey Kamwela amekiri kuwepo tukio hilo na kuongeza kuwa Polisi wanaendelea na uchunguzi zaidi wakati mtuhumiwa akishikiliwa.
Kwa mujibu wa Dk Kitundu, mtuhumiwa alikiri kutokuwa na cheti kutoka chuo chochote cha afya na kwamba alikuwa akiendesha shughuli za kutoa matibabu kwenye duka lake la dawa.
Dk Kitundu alisema tukio hilo ni la Agosti 10 mwaka huu saa 4 asubuhi katika Kijiji cha Iyumbu wilayani Ikungi ambapo inadaiwa kuwa Jubulu alifariki muda mfupi baada ya kupewa matibabu na Samson. Taarifa za awali zinadai, alimzidishia mgonjwa huo kipimo cha dawa.
Kulingana na maelezo ya Dk Kitundu, Jubulu alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya kifua, kiuno na mgongo hivyo baada ya kupewa dawa husika, alipoteza fahamu.
“Baada ya kubaini hali ya mteja wake inakuwa mbaya kutokana na kumzidishia dozi, alimpatia chupa tisa za maji ili kuokoa maisha yake lakini juhudi hizo hazikuzaa matunda hadi mauti kumfika,” alisema Dk Kitundu.
Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya alisema, alipata taarifa za tukio hilo Agosti 11 mwaka  huu na kwamba alipoenda kufanya ukaguzi kwenye duka hilo la dawa, aligundua mtuhumiwa hakuwa na leseni kutoka Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA)  ya kumruhusu kufanya biashara ya kuuza dawa kwa ajili ya binadamu.
“Nilikuta dawa  mbalimbali ambazo haziruhusiwi kwenye maduka ya dawa muhimu na nyingine zilizoisha muda wake wa matumizi,” alisema Dk Kitundu.

No comments: