CCM YABANA MAWAZIRI BUNGE LA KATIBAChama Cha Mapinduzi(CCM) kimewabana mawaziri na wabunge wake wasiohudhuria shughuli za Bunge Maalumu la Katiba.
Moja ya hatua iliyochukuliwa na chama hicho tawala ni kupunguza idadi yao   kwenye ziara ya Rais Jakaya Kikwete aliyoianza jana mkoani Morogoro.
Vilevile mawaziri wote wasiokuwa na shughuli za msingi au za lazima wametakiwa lazima kuhudhuria vikao vya kamati na mjadala wa bunge hilo tofauti na sasa wengi ambapo wengi wao wamekuwa hawahudhurii kabisa au wanahudhuria mara chache.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Halmashauri Kuu(NEC) ya CCM, Nape Nnauye alibainisha hayo wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari waliotaka kufahamu msimamo wa Kamati Kuu (CC) kuhusu mawaziri na wabunge
wasiohudhuria bunge hilo.  
Nnauye alikuwa akitoa maelezo ya kilichojiri kwenye CC iliyokutana juzi mjini hapa chini ya Mwenyekiti wa chama hicho, Jakaya Kikwete kujadili Maendeleo ya Mchakato wa mabadiliko ya Katiba nchini ndani ya nje ya bunge hilo.
Akizungumzia kilichojiri kwenye CC ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Katibu huyo wa Itikadi alisema imeridhishwa na juhudi za vyama vya siasa na wadau katika kujenga na kuimarisha maridhiano na mshikamano kwa lengo la kupata muafaka, lakini imesikitishwa kuvunjika kwa mazungumzo kati ya CCM na vyama vya upinzani vinavyounga Ukawa (Umoja wa Katiba ya Wananchi) ambavyo ni CUF, Chadema na NCCR Mageuzi yaliyokuwa yanasimamiwa na Msajili wa vyama vya siasa nchini, Jaji Francis Mutungi yakiwa na lengo la kupata maridhiano.
“Kamati Kuu imepokea na kuridhishwa na taarifa kuhusu juhudi zinazofanywa na TCD(Baraza la Demokrasia nchini) na vyama vinavyounda TCD katika kutafuta muafaka wa kisiasa kwa lengo la kuimarisha amani, utulivu, mshikamano na kuaminiana kati ya wadau mbalimbali na hasa kati ya vyama vya siasa”, alisema. 
Kamati Kuu hiyo imemuagiza Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana pamoja na kazi nzuri anayofanya kukiwakilisha chama hicho kwenye vikao vya maridhiano kuendelea kukutana na vyama hivyo na wadau wengine katika kufanikisha lengo la maridhiano ili kupatikane katiba mpya.
Pamoja na hayo CC imeridhishwa na mwenendo wa Bunge la Katiba na majadiliano na upigaji kura katika kamati hizo za bunge hilo.
 “Kamati kuu imeridhishwa namna wajumbe wa Bunge Maalumu wanavyoshiriki katika kujadili na kujenga hoja na wanavyoshughulikia tofauti za kimtazamo na kimawazo katika vikao vyao na uhitimishaji wa majadiliano kwa kura…CC inawahimiza wajumbe wa bunge kushiriki kwenye mijadala kwa kutanguliza maslahi mapana ya taifa na kuipatia nchi katiba inayotarajiwa na watanzania wote,”alisema.

No comments: