BUNGE LA KATIBA KUANZA BILA WAJUMBE WA UKAWA

Bunge Maalumu la Katiba litaendelea na vikao bila kujali uwepo au kutokuwapo kwa baadhi ya wajumbe waliojiundia kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge),  William Lukuvi, ambaye ndiye Mratibu wa Bunge hilo, alitoa kauli hiyo jana wakati wa mdahalo ulioandaliwa na Jumuiya ya Wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udasa).
Alikuwa akijibu hoja iliyowasilishwa wa wachangia mada mbalimbali, kuhusu kusitishwa kwa Bunge hilo kupisha Uchaguzi Mkuu ufanyike, kisha mchakato uanze upya katika Serikali ya Awamu ya Tano.
Hoja nyingine kama hiyo ambayo Lukuvi aliitolea jibu hilo, ni ya kusogezwa mbele kwa Bunge Maalumu la Katiba, ili kutoa muda kama wa wiki moja wa kushawishi zaidi wajumbe wa Ukawa, kurejea katika Bunge hilo.
“Ukawa wasipofika bungeni hatutasitisha Bunge, tuliopo tunatosha, tutajadilina na kufikia makubaliano na kuja kuwaeleza wananchi ingawa haitakuwa na afya sana,” alisema Lukuvi katika mdahalo huo ambao mada ilikuwa  ‘Nini kifanyike Bunge Maalumu la Katiba liendelee’.
Lukuvi alirejea kauli ya mtoa mada, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wasira, kuwa mjadala wa Bunge hilo litakaloanza kesho, utahusu mahitaji ya maisha ya Watanzania na sio idadi ya Serikali, wala mgawanyo wa madaraka.
Alifafanua kuwa mjadala utahusu kama watoto wa Watanzania wapewe elimu bure au la, namna ya kugawana kwa haki rasilimali za Taifa, maji, afya na masuala kama ya ardhi na uchumi.
Kwa mujibu wa Lukuvi, haoni sababu wala mantiki ya wajumbe wa Ukawa, kususa kujadili mambo yanayohusu wananchi kwa kuwa suala la idadi ya Serikali, halitakuwepo.
Wasira alisema mjadala wa kipengele cha muundo wa serikali ulishafungwa na kuwa Bunge Maalumu litajadili sura 15 za Rasimu ya Katiba zilizobakia, zinazohusu maisha ya Watanzania.
“Suala la Serikali tatu au mbili tulishamaliza, tunakwenda kuzungumza mambo ya msingi yanayohusu jamii, tunakwenda kuzungumzia haki za wanawake, uchumi wa nchi unavyoendeshwa, hivyo Ukawa waje tujadili vifungu vilivyobaki," alisema Wasira.
Wasira alimshukuru Rais Jakaya Kikwete, kwa kuwa mwepesi wa kubadilika na kuwa msuluhishi na msikivu wa hoja tangu mchakato wa Katiba ulipoanza.
Katika hatua nyingine, mtoa mada, Dk Kitila Mkumbo, alikiri kuwa hatua ya Rais Kikwete kukubali kuanzisha mchakato huo, ni ya mafanikio makubwa na ameingia katika historia, kwa kuwa hakuna Rais wa Tanzania aliyemtangulia, aliyewahi kuchukua hatua hiyo kubwa.
Hata hivyo, Dk Kitila alitaka Rais Kikwete ashawishiwe kusitisha mchakato huo, kutokana na hali iliyofikiwa, ili pamoja na mambo mengine, atoe nafasi ya kufanyika kwa  Uchaguzi Mkuu ujao, kisha Rais ajaye auendeleze.
Mchangiaji, Profesa Anna Tibaijuka, alisema Rais Kikwete ameibuka mshindi katika mchakato huo, kwa kutimiza matakwa ya demokrasia ya kusikiliza wachache, kwa kuwa alianzisha mchakato huo, ingawa haukuwa katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2010.
Alisema kama Rais asingechukua uamuzi huo, elimu kuhusu mchakato wa Katiba iliyopatikana mpaka sasa, isingepatikana.
Mtoa mada, Tundu Lissu, ambaye ndiye Msemaji wa Ukawa, alisisitiza nia ya wajumbe wa kundi hilo ya siku nyingi ya kususa Bunge Maalumu la Katiba.
Alisema hawataingia bungeni na kuwa endapo Bunge litapitisha Katiba inayopendekezwa, wao wataendelea na mapambano ya kutaka Katiba mpya wakiwa nje ya Bunge.
“ Posho hizo hatutaki, mtakayoyajadili na kuyapitisha, kesho yake tutaendeleza mapambano ya kutaka Katiba mpya, hoja yetu ni kupata Katiba mpya na sio kalamu ya chama,” alisema.
Profesa Gaudence Mpangala wa Chuo Kikuu cha Ruaha, alisema utafiti uliofanywa, ulibaini chanzo cha kuvurugika kwa mchakato wa Katiba, ni kutozingatia misingi ya rasimu ya Katiba iliyowasilishwa.
Sababu zingine alitaja kuwa ni hali ya kubeza na kuiponda rasimu na mazingira ya ufunguzi wa Bunge na mjadala kugubikwa na lugha za matusi, kebehi, kubaguana na lugha za kukashifiana.
Akizungumzia ufumbuzi wa tatizo hilo, Profesa Mpangala alitaka mjadala uzingatie maoni ya wananchi, wabunge kuwa na mtazamo wa kitaifa na kwa manufaa ya vyama vyao.
Aliwataka Ukawa kurejea bungeni. Alisema endapo Ukawa wataendelea na msimamo wa kutorejea bungeni, basi wanasheria waangalie mwanya wa kanuni wa kusitisha vikao vya Bunge hadi baada ya uchaguzi mkuu 2015.
Wakati limesitishwa, Profesa Mpangala alitaka Bunge la Jamhuri ya Muungano, lirekebishe sheria kadhaa, zitakazotumika katika uchaguzi ujao na Bunge la Katiba, liundwe upya kwa kurekebisha kasoro zilizopo, ikiwamo kupunguza idadi ya wanasiasa, iwe theluthi moja ya wajumbe.
Dk Mkumbo katika mada yake, alisema mchakato wa Katiba mpya ni kama umeshindwa, kutokana na pande mbili za Ukawa na CCM kushindwa kufikia maridhiano na kila upande kusimamia msimamo wake.
Alisema mchakato huo, pia umeshindwa kuendelea, kutokana na wajumbe wa Bunge Maalumu, kutokuwa na  weledi na umakini wa kuandika Katiba mpya, hasa kutokana na mwenendo ulionekana katika awamu ya kwanza ya Bunge hilo.
“Hawana weledi wa kuandika Katiba na wamekosa weledi ambao uko katika kushindwa kukabiliana na hoja kinzani, kwani kila mtu anataka kusikia hoja yake na kuisikia sauti yake,” alisema.
Alitaka mchakato huo, uahirishwe hadi baada ya Uchaguzi Mkuu ili Bunge Maalumu liundwe upya, kwa kuwa na theluthi moja ya wajumbe ambao ni wanasiasa.
Katika Bunge hilo jipya, Dk Mkumbo pia alipendekeza kuwa wajumbe wake watakiwe wasigombee uchaguzi ujao, kwani baadhi ya wajumbe wa sasa, wamekuwa wakitumia mjadala huo kujipatia umaarufu.
Pia, alitaka Wazanzibari waulizwe kama wanataka Muungano au la, kwani nchi inapokubali Muungano ni lazima wajue kuwa kuna haki, ambazo inapoteza kwa kuwapo katika Muungano.
Alisema haiwezekani nchi ikawa huru ndani ya Muungano, au ikawa na Mkataba katika Muungano na kuendelea kuwa huru.
Wasira katika mada aliyotoa, alisema: “Tatizo la wenzetu (Ukawa) ni serikali tatu au mbili, lakini kwa sababu Katiba ni zaidi ya tatu na mbili, kuna mambo ya msingi tunarudi Dodoma kuyashughulikia na kuyazugumza.
“ Suala la serikali tatu au mbili tulishamaliza, tunakwenda kuzungumza mambo ya msingi yanayohusu jamii, tunakwenda kuzungumzia haki za wanawake, uchumi wa nchi unavyoendeshwa, hivyo Ukawa waje tujadili vifungu vilivyobaki."
Akifunga kongamano hilo,  Lukuvi alisema mtu mwenye ushawishi mkubwa ndani ya Ukawa, ni Lissu na kumuomba alegeze msimamo ili warejee bungeni.
 “Ninakuomba Lissu maana wewe ni mzizi wa Ukawa… unaweza kujifungia saa sita mpaka 24 bila kula kwa ajili ya kujenga hoja, sasa nakuomba kawashawishi warejee bungeni,” alisema.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Mwigulu Nchemba, alisema sababu ya kukwama kwa Bunge la Maalum la Katiba, ni kutawaliwa na dhambi ya ubinafsi kwa vyama, kutumia wananchi kama kichaka cha kupitisha mambo binafsi.
“Tumefanya dhambi ya ubinafsi na hili limefanywa na vyama vyote na tulianza kwa kuwa na vikao vya kivyama ambako tulikwenda kuweka misimamo ya vyama, tumeshinda hata kutumia viongozi wetu kutushauri pale tulipokwama na hatuwezi kusubiri tukodi watu kutoka nje ili watupatanishe.
“ Pia kuna dhambi ya kuwageuza wananchi kuwa kichaka cha kupitisha mambo yao, hivi kweli wananchi walitaka tulipwe Sh 300,000?.
“ Ukawa warudi na tufike mahali tujifungie na kukubaliana, kama ni serikali tatu au tukubaliane kurudisha kodi ya mbwa ili tupate fedha za kuendesha serikali tatu, lakini tupitishe mambo kwa umoja na tusiwapeleke Watanzania kama nyumbu,” alisema Mwigulu.
Akijibu swali la kwanini CCM haitaki kukubaliana na hoja ya kuwa na serikali tatu, Mwigulu alisema chama chake hakijaona sababu za msingi za kuvunja muundo ulioafikiwa na waasisi wa Taifa.
“ Ukawa, hii ni aibu Bunge kuendelea bila kuwapo au livunjike kwa sababu yenu, tumekomboa nchi nyingi na tumekuwa wasuluhishi, leo hii tukashindwa kwenye jambo hili,” alisema.
***************************

No comments: