ANAYEDAIWA MFUASI WA AL SHABAAB APELEKWA KWA DCI


Mshitakiwa anayekabiliwa na kesi ya kuwa mwanachama wa kundi la kigaidi la Al Shabaab, Mussa Mtweve,  amepelekwa kwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) kwa ajili ya mahojiano.
Hakimu Mkazi, Emilius Mchauru alitoa amri hiyo jana baada ya kukubali ombi la upande wa Jamhuri wakati kesi hiyo ilipotajwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Akiwasilisha ombi hilo, Wakili wa Serikali Aldo Mkini alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na DCI ameomba Mtweve apelekwe ofisini kwake kwa ajili ya mahojiano.
Hakimu Mchauru alikubali ombi hilo na kuahirisha kesi hadi Agosti 18, mwaka huu itakapotajwa tena.
Mbali na Mtweve washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Ally Rashid, Shaban Waziri na Faraji Ramadhani.
Inadaiwa  kati ya Januari 11, mwaka juzi na Septemba 16, mwaka jana, eneo la Kibaoni, Dar es Salaam, Rashid alisajili watu hao (washitakiwa wenzake) kuwa wanachama wa kundi hilo.
Alidai katika siku hizo, walikamatwa kwa kuwa wanachama wa kundi la kigaidi la Al Shabaab nchini. Kundi hilo linafanya shughuli zake Kenya na Somalia.
Washitakiwa hao wanaendelea kusota rumande kutokana na mashitaka yao kutokuwa na dhamana.

No comments: