ZITTO KABWE AKANA KUWA MWANACHAMA WA UKAWA

Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (Chadema) amesisitiza hajawahi kuwa katika kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) wala kundi lolote ndani ya Bunge Maalumu la Katiba isipokuwa, yuko kwenye linalotaka maridhiano.
Hata hivyo katika taarifa yake kwa vyombo vya habari aliyoitoa jana, Zitto alisema msimamo wake kuhusu mchakato wa kuandika Katiba mpya ni  kutohudhuria Mkutano wa Bunge Maalumu unaotarajiwa kuanza wiki ijayo, kama makundi hasimu hayatafikia maridhiano.
Alisisitiza msimamo wake kuhusu Muungano kuwa ni serikali tatu zilizoboreshwa kuwa na Muungano imara usio tegemezi wala egemezi kwa washirika wake.
Mbunge huyo alikuwa akitoa kile alichosema ni ufafanuzi kuhusu msimamo wake kulingana na mahojiano aliyofanyiwa katika kipindi cha PowerBreakFast kinachorushwa na Clouds FM na hatimaye, mahojiano hayo kuandikwa na baadhi ya vyombo vya habari.
Alisema Mkutano wa Bunge Maalumu utakaofanyika bila kuwepo kwa maridhiano utakuwa hauna maana yoyote na itakuwa ni sawa na kupoteza muda na fedha za walipa kodi ambazo zingeweza kununua dawa vijijini.
Hata hivyo, Zitto alisema anaunga mkono mgomo wa baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kupinga lugha za matusi na lugha za kibaguzi zilizokuwa zinaendelea ndani ya mikutano.
Pia alisema anaunga mkono kwamba Rasimu inayopaswa kujadiliwa ni iliyotokana na Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba.
Zitto alisema kwa hali ya sasa kuna mkwamo katika kupatikana kwa Katiba bora, unaotokana na kutokuwepo kwa nia ya dhati ya kupata maridhiano ya pande zinazopingana.
“Ukawa hawataki mazungumzo na viongozi wa Bunge la Katiba badala ya kujenga maridhiano kila siku wanawabeza Ukawa, jambo ambalo kamwe haliwezi kujenga mwafaka.
“Ushauri wangu ni kuahirisha mchakato mzima wa kuandika Katiba mpaka mwaka 2016 baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015. Katiba ya sasa ifanyiwe marekebisho machache,”  alisema katika taarifa yake. 
Kwa mujibu wa Mbunge huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), aliyataja marekebisho yanayotakiwa kufanywa kwenye Katiba ya sasa kuwa ni pamoja na Tume ya Uchaguzi kuwa huru kwa kuwaondoa watumishi wa Halmashauri za Wilaya, Miji na Majiji katika kusimamia uchaguzi.
Marekebisho mengine ni,kuruhusu mgombea binafsi na kuondoa mafuta na gesi kama jambo la Muungano ili Zanzibar ianze mara moja kusimamia kwa uhuru utafutaji wa mafuta katika vitalu vilivyopo upande huo wa Muungano.

No comments: