WALIOFARIKI, MAJERUHI AJALI YA BASI LA MOROBEST HAWA HAPA

Ajali  ya watu 19 wamekufa katika ajali mbili tofauti zilizotokea mkoa wa  Dodoma na Arusha jana.
Ajali hizo mbili zimesababisha majeruhi zaidi ya 70.
Ajali ya kwanza mbaya ilihusisha basi la abiria na lori ambapo watu 17 walikufa na wengine 56 kujeruhiwa. Katika ajali hiyo basi la abiria na lori yaligongana uso kwa uso.
Aidha,  katika ajali ya Arusha, madereva wa magari mawili yaliyogongana maeneo ya Sadeki wilayani Arumeru, walikufa na wakati huo huo watu 14 wamejeruhiwa.
Ajali ya mkoani Dodoma ilihusisha basi la Morobest lililokuwa likitoka Mpwapwa kwenda Dar es Salaam, na ilitokea eneo la Pandambili, Wilaya ya Kongwa.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, David  Misime alisema ajali hiyo ilitokea saa 2 asubuhi jana. Kati ya 17 waliopoteza maisha,  wanaume ni 12.
Basi hilo lenye namba za usajili T258 AHV likiendeshwa na Said Lusogo, liligongana na lori namba T820CKU/ T390CKT likitoka Dar es Salaam kwenda Dodoma,  likiendeshwa na Gilbert  Nemanya. Madereva wote wawili wamekufa.
Kwa mujibu wa Kamanda Misime, kufikia jana mchana miili  11 ilikwishatambuliwa.
Waliotambuliwa ni  dereva wa lori hilo, Nemanya  pamoja na utingo wake, Mikidadi Zuberi.
Wengine ni dereva wa basi la Morobest, Lusogo na kondakta wake, Omary Mkubwa.
Marehemu wengine waliotambuliwa ni Merina Malikeli, Nasib Machenje, Wilson Suda, Gabriel Mejachiwipe, Justine Makasi na mwanamke aliyetambuliwa kwa jina moja la Christina.
Kwa mujibu wa Misime, watu 56 wamepata majeraha mbalimbali na wamelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kongwa na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.
Alisema chanzo cha ajali hiyo ni dereva wa lori kutokuwa na hadhari kwa magari yaliyokuwa yanakuja mbele yake wakati anapita gari lingine.
Majeruhi 23 wamelazwa katika hospitali ya Mkoa wa Dodoma.
Majina yao ni Frank Raymond, Patricia Ngamwai, Amos Chiwaga, Mary Mateo, Safari Jonas, Suzan Charles, Gasper Shao,Felician Rite, Felister Mathias, Amos Jonas, Edina Lwande, Seleman Kaseni, Nazareth Kasua, Saimon Msoloka, Juma Mtezi  na   Swalehe Bakari.
Wengine ni Naseria John, Getruba Kombo, George Njelewa, Manase Makuja, Chibago Mchiwa, Nicholous Roger na Michael Chibwela.
Kwa upande wa ajali ya mkoani Arusha, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas alisema ilitokea juzi saa 3 usiku maeneo ya Sadeki kwa Fundi.
Alisema gari aina ya Subaru lenye namba za usajili T842 CCP lililokuwa likiendeshwa na David Natal (35) liligongana na gari ya Nissan Mini Bus lenye namba za usajili T355 CGA lililokuwa likiendeshwa na aliyetambuliwa kwa jina moja la Joshua.
Alisema ajali hiyo ilitokea wakati Natal aliyekuwa anatoka Arusha mjini kwenda Makumira, alipojaribu kupita  gari lililokuwa mbele yake ndipo lilipogongana na gari lililokuwa linatoka Usa River kwenda Arusha mjini.
Mbali na vifo vya madereva hao, ajali hiyo ilisababisha majeruhi 14 waliokuwa kwenye gari aina ya Nissan Mini Bus.
Majeruhi hao ni Frida Joseph (18), Elisante Mungure (45), Lilian Mathias (29), Juma Mohamed (42), Silvia Kelvin (26), Charles Massawe (40), Kelvin Charles (29), Emmanuel Adedia (29), Zainabu Issa (40), Regard Joseph (30), Elirehema  Abrod (29),  Alfred Lucas (21), Gipson Tackson (3) na Salma Abdallah (44).
Kamanda alisema majeruhi hao wanatibiwa katika Hospitali ya Tengeru na Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru.

No comments: