WALIMU WANNE WATIMULIWA KAZI KWA MAPENZI NA WANAFUNZI

Walimu wanne wa kiume wa Shule ya Sekondari Mwembetogwa ya mjini Iringa, wamefukuzwa kazi baada ya kubainika wakijihusisha na uhusiano wa kimapenzi na wanafunzi.
Walimu  hao walifukuzwa  kazi takribani miezi mitatu iliyopita.
Pia,  shule hiyo ya Jumuiya ya Wazazi,  imefukuza wanafunzi wawili wa kike, kwa madai kukubuhu katika ngono. 
Mkuu wa Shule hiyo, Kevin Mlengule alisema walimu na wanafunzi hao, walibainika kujihusisha na vitendo vinavyobomoa maadili ya watumishi na wanafunzi, baada ya kupigiwa kura ya siri.
“Katika kuboresha nidhamu kwa watumishi na wanafunzi wawapo shuleni, jambo lililokuwa linatusumbua na tukaamua kulitafutia dawa kali ni la mahusiano ya mapenzi kati ya walimu na wanafunzi, na wanafunzi na watu wa mitaani,” alisema.
Alisema miaka mitatu iliyopita, lilikuwa ni jambo la kawaida kwa wanafunzi wa kike, kujihusisha katika mapenzi na walimu wao pamoja na watu wengine kutoka mitaani.
 Hali hiyo ilisababisha baadhi ya wanafunzi wenye tabia hiyo, kufuatwa na wanaume shuleni muda wowote na kutoroshwa; vitendo vilivyoporomosha taaluma.
Mlengule alisema matokeo hayo, yaliwafanya baadhi ya wazazi kuwahamisha watoto wao kutoka shule hiyo.
“Shule ilikuwa na wastani wa wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha sita 2,500 kila mwaka, matatizo hayo na mengine yaliyokuwepo, yaliifanya ibakiwe na wanafunzi wasiozidi 600,” alisema.
 Alisisitiza “hatuna mzaha hata kidogo, mwalimu na mwanafunzi atakayebainika akijihusisha na ngono katika mazingira yoyote yale, wote kwa pamoja tunawafukuza.”
 Alisema udhibiti huo, umewezesha ufaulu katika shule hiyo kuongezeka. Alisema matokeo ya kidato cha sita mwaka 2012, 2013 na 2014 ni kielelezo tosha.
 Alisema katika matokeo ya mwaka huu, hakuna mwanafunzi aliyefeli kati ya wanafunzi 156 waliofanya mtihani wa kidato cha sita.
Matokeo hayo yamefanya shule hiyo kuwa ya kwanza kati ya shule sita za kidato cha sita zilizo katika Manispaa ya Iringa. Imekuwa ya sita kimkoa kati ya shule 22. Kitaifa ni ya 47 kati ya shule 268.
Baadhi ya wazazi walipongeza uamuzi huo wa shule. “Tunataka shule nyingine ziige mfano wa shule hii, tumefarijika kusikia imechukua uamuzi huo na kwa kufanya hivyo, tunaamini shule hiyo itakuwa salama kwa watoto wetu wa kike,” alisema mmoja wa wazazi, Joachim Mwaikambo.

No comments: